MISA TAN YATOA TAMKO MWANDISHI DICKSON NG’HILY KUNYANYASWA AKIPIGA PICHA WANAFUNZI WAKISOMEA CHINI YA MTI


 TAARIFA YA KUPINGA HATUA ZA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI NA UNYANYASAJI DHIDI YA MWANDISHI DICKSON NG’HILY. 

Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA TANZANIA),imepokea taarifa za kupigwa kujeruhiwa,kunyang'anywa simu na kuharibiwa simu yake Mhariri wa Habari wa Biashara na Mkuu wa Kitengo cha Digital cha Kampuni ya The Guardian Limited, Bw. Dickson Ng’hily. 

Mhariri huyo ambaye ni mwandishi wa habari alikuwa katika utekelezaji wa majukumu ya kazi za uandishi wa habari kwa kupiga picha wanafunzi wa shule ya msingi Kwembe,Manispaa ya Ubungo mkoani Dar es Salaam, waliokuwa wanasomea chini ya mti. 

Katika tukio hilo, mwandishi alishambuliwa na wanafunzi ambao walipata maelekezo kutoka kwa mwalimu wao jambo ambalo halikuwa sahihi. 

Katika dunia ya ukuaji wa tekonolojia kuzuia mwandishi wa habari kupiga picha ni sawa na kuzuia mabadiliko kwa kuwa picha zinaweza kupigwa kwa namna nyingi bila muhusika kufika eneo husika.

 MISA TANZANIA tunakemea uamuzi wowote wa kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa ni kinyume cha sheria. 

Pia licha ya mwandishi huyo kujitambulisha na kuonesha vitambulisho vyake lakini bado aliendelea kushambuliwa kama mhalifu. Kitendo hiki hakikubaliki kwa kuwa kinakwenda kinyume na sheria na kusigina uhuru wa kupata taarifa na uhuru wa vyombo vya habari. 

Tunatoa wito kwa wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi kwa kumpiga na kumjeruhi binadamu,lakini mamlaka za serikali zilizohusika na ukamataji kuhakikisha haki inatendeka. 

Pia tunawakumbusha waandishi wa habari kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria,kanuni na taratibu za nchi.

 Imetolewa na MISA TANZANIA.

 Julai 12, 2024 Dar es Salaam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post