VIKUNDI VYA HISA KUWASAIDIA WATU WENYE ULEMAVU KUJUA HAKI ZAO
KWA muda mrefu watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa elimu ya masuala ya kifedha kulingana na hali zao jambo ambalo linawafanya kushindwa kushughulikia vikwazo vyao katika jamii.


Katika kubakiliana na hilo, jumla ya vikundi 20 vya kuweka na kukopa vya watu wenye ulemavu vimeanzishwa kwa lengo la kujiendeleza kiuchumi na kuondokana na utegemezi kupitia mradi wa KIJALUBA iSAVE unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Shirikisho la Jumuiya za Watu wenye Ulemavu Zanzibar na Chama cha Watu wenye ulemavu nchini Norway (NAD) katika Mkoa wa Kusini Unguja.


Vikundi hivyo vinavyoundwa na idadi ya wanachama 30 vikijumuisha wanawake na wanaume, wanachama wamewezeshwa kuanzisha na kujishughulisha katika miradi mbalimbali ya ujasiriamali ikiwemo utengenezaji wa sabuni na mafuta ya mwani bila kujali hali zao za ulemavu.

Baadhi ya vikundi vilivyoanzishwa ni pamoja na TUTAMBUWANE kilichopo Jambiani Mkadini, MWANZO MGUMU Michamvi Kae na kikundi cha NYOTA YA BAHATI kilichopo shehia ya Bwejuu.

Afisa Msaidizi wa mradi huo kutoka TAMWA ZNZ, Khairat Haji alisema mradi umetoa mafunzo mbalimbali kwa vikundi hivyo kwa lengo la kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu kujua haki zao na kukabiliana na vikwazo mbalimbali katika jamii.


Alieleza wanufaika wamejengewa uwezo wa elimu ya kuweka na kukopa kwenye vikundi, umuhimu wa kuweka akiba, jinsi ya kutumia mikopo, elimu ya biashara na mbinu za kuendesha biashara zao kwa kulingana na hali zao.


"Tumetoa mafunzo mbalimbali kwa lengo la kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu kujua haki zao, umuhimu wa kuweka na kukopa na jinsi ya kutumia mikopo na kufanya biashara na kuziendesha,"alieleza Khayrat Haji, Afisa Msaidizi wa Mradi wa Kijaluba.

“Lengo kuu la mradi limefanikiwa kwa kiasi kwa sababu haikuwa jambo rahisi kubadilisha mitazamo iliyojengeka katika jamii kwamba watu wenye ulemavu ni wa kupokea zaidi misaada badala ya kujishughulisha na kujiongezea kipato katika kujikwamuwa kiuchumi, Khayrat", alisema.


Naye Afisa uwezeshaji kiuchumi kupitia mradi wa KIJALUBA iSAVE, Muhidin Ramadhan Muhidin alisema mradi unaendelea na zoezi la kuvisajili vikundi vyote vilivyopo chini ya mradi huo kupitia Idara ya Ushirika ili viweze kutambulika kisheria.


Alibainisha, “lengo la kuvisajili vikundi hivyo ni kupata fursa ya kufungua akaunti Benki na kuhifadhi fedha zao ili ziwe katika mazingira bora na salama,” alieleza Muhudin.


Ramadhani Haji, Mwenyekiti wa Kikundi cha Ushirika TUTAMBUWANE alieleza uwepo wa mradi umewasaidia watu wenye ulemavu kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili wao wenyewe ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto na kuhudumia matibabu ya wagonjwa.


“Kupitia mfuko wa jamii, fedha zetu tunazoweka tumetatua matatizo mbalimbali. Tulipata maafa baadhi ya nyumba zetu kuingia maji na tukapata mkopo, pia wagonjwa waliolazwa walifaidika na mkopo huo kupitia jamaa zao waliojiunga kwenye vikundi," alieleza mwana kikundi huyo.


Kijaluba iSAVE Zanzibar ni mradi jumuishi unaotekelezwa Zanzibar na TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na SHIJUWAZA na Chama cha Watu wenye ulemavu nchini Norway (NAD) katika wilaya mbili za Chake chake kwa upande wa Pemba na Kusini kwa Unguja ukiwa na lengo la kuwezesha watu wenye ulemavu na kuwajengea uwezo kuhusu mitazamo chanya ya ushiriki katika shughuli za kujipatia kipato kupitia vikundi vya kuweka na kukopa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post