SERIKALI YAWAHAKIKISHIA WADAU WA SEKTA YA HABARI KUWA WAPO KWENYE MIKONO SALAMA

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) 

Na Mwandishi Wetu,Dar Es Salaam

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) amewahakikishia wadau wa sekta ya habari kuwa sekta ipo kwenye mikono salama.

Waziri Nape ametoa ahadi hiyo tarehe 19 Juni, 2024 wakati akifunga Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari lililofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 18 hadi 19 Juni, 2024, kwenye ukumbi wa mikutano wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Mhe. Nnauye ameeleza kuwa Kongamano hilo limewaunganisha wadau wote wa sekta ya habari na limechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ukuaji wa sekta hiyo.

“Wanahabari niwahakikishie kuwa Sekta ya Habari ipo mikono salama. Tuweke utamaduni wa kujadiliana vitu vitakavyoleta maendeleo katika nchi yetu. Kwa siku mbili tulizokuwa hapa tumejenga misingi bora zaidi, tumepata fursa ya kujadiliana mambo mbalimbali”.

Alifafanua kuwa sekta ya habari ni muhimu katika kuleta mageuzi ya kiuchumi, kijamii na hata kisiasa, hivyo wanahabari wakiamua, wana uwezo wa kurahisisha na kuchochea maendeleo ya Taifa kwa kasi zaidi.

Pia Waziri Nape ameishukuru Kamati aliyoiundwa kutathmini hali ya uchumi wa vyombo vya habari ikiongozwa na Bw. Tido Mhando kwa kazi nzuri waliyoifanya na kuahidi kuwa yote yaliyowasilishwa kwenye ripoti yao yatafanyiwa kazi.

“Niombe ripoti hii iwe chanzo cha mijadala zaidi. Ninaamini ripoti hii haiwezi kuwa muarobaini wa matatizo ya wanahabari lakini ni mwanzo mzuri kuelekea mabadiliko tunayoyatamani. Niwaombe wadau wengine walioguswa na ripoti hii waangalie yanayowahusu na wayafanyie kazi” amesisitiza Mhe. Nnauye.

Wakati huo huo, Mhe. Nnauye amewaeleza wadau wa sekta ya habari kuwa mambo yote waliyokubaliana yatafanyiwa kazi na yanayowezekana kufanyiwa kazi kwa sasa yatafanyiwa na yasiyowezekana kwa sasa yatafanyiwa kazi kwa wakati sahihi.

“Wanahabari wenzangu niwahakikishie mimi ni muumini wa uhuru wa vyombo vya habari. Mada zilizowasilishwa na maazimio tuliyojiwekea yakawe chachu ya maendeleo ya sekta yetu. Nataka niwahakikishie wanahabari nyinyi ni wadau na si washindani wa Serikali” amesema Mhe. Nnauye.

Kongamano la Pili la Maendeleo ya Sekta ya Habari limehusisha wahariri wa vyombo vya habari, waandishi wa habari na maafisa habari wa Serikali, likibeba kauli mbiu ya ‘Jenga mustakabali endelevu kwenye sekta ya habari katika zama za kidijiti’.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post