MATUMIZI YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA KUCHOCHEA MAENDELEO ENDELEVU_ MAJALIWA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa,akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu jijini Tanga

.........

#Akoshwa na Ubora wa Maonesho

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema rasilimali watu yenye elimu, ujuzi, weledi na maarifa ndio msingi wa kujenga uchumi shindani na endelevu.

Mhe. Majaliwa amesema hayo Mei 31, 2024 jijini Tanga wakati akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu akisema kuwa Serikali inalenga kuongeza mikakati na hamasa ya kukuza elimu, ujuzi, na matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu (STU) kama nyenzo za kusaidia kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii pamoja na kuchagiza maendeleo ya nchi kwa ujumla.

‘’Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuendeleza elimu ngazi zote msingi, elimu ya ufundi, Elimu ya Juu pamoja na shughuli za utafiti na ubunifu," amesema Mhe Majaliwa.

Amepongeza maandalizi ya Maadhimisho hayo kuwa ya viwango vya juu na kuagiza kutangazwa pia kimataifa huku akifurahishwa na ushiriki wa wadau mbalimbali katika kuendeleza sekta ya Elimu Sayansi na Teknolojia kupitia Wizara na Taasisi zake.

"Nimefurahi sana kuona ushiriki wa Wadau wa Maendeleo na Sekta Binafsi kupitia mradi niliouzindua wa Smart Wasomi mnaotekekeza kwa ushirikiano, Serikali itaendelea na kazi ya kuvutia fedha na rasilimali nyingine kutoka kwa Wadau wa Maendeleo na Sekta Binafsi ili kuongeza fursa za utoaji Elimu uendelezaji ujuzi na kuimarisha matumizi ya teknolojia’’ Alisema Majaliwa.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema katika kuongeza mchango wa sayansi, teknolojia na ubunifu, Wizara inaendelea kutekeleza juhudi mbalimbali ikiwemo kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia yanayolenga kuiboresha na kuihuisha kuwa Sera ya Taifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.

"Kuna bunifu na teknolojia zenye sifa na zinajibu changamoto za kiuchumi na kijamii, hivyo, Wizara itaendelea kuchukua hatua zinazolenga kuziendeleza na kuzibiasharisha" amebainisha Mkenda.

Aidha Waziri huyo amesisitiza azma ya Serikali ya kuendeleza ujuzi ambapo katika Maonesho hayo vijana walishiriki na kushindanishwa katika umahiri wa kazi za ujuzi na washindi watano watashiriki katika ngazi ya kikanda.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Michezo na Utamaduni Mhe. Husna Sekiboko amesema Bunge linajivunia kazi nzuri zilizofanywa na Wizara ya Elimu Sayandi na Teknolojia katika Maonesho hayo na kwamba bunifu za mwaka huu zimejikita katika kutatua changamoto zilizopo katika jamii.

Maadhimisho ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu Mwaka 2024 yamefanyika Mkoani Tanga kuanzia tarehe 25 hadi 31 Mei na kuleta pamoja Taasisi na Vyuo zaidi ya 320 kuoesha bunifu, teknolojia zilizozalishwa tafiti na kutoa elimu na huduma kwa wananchi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post