MADIWANI MANISPAA YA TEMEKE WAMEUSHUKURU UONGOZI WA KITUO CHA UHUSIANO WA KIMATAIFA CHA DKT. SALIM AHMED SALIM KWA KUWAPATIA MAFUNZO

 


Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam 

Naibu Meya wa Manispaa ya Temeke Mheshimiwa Arnold Emmanuel Peter ameushukuru Uongozi wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kwa kutoa mafunzo kwa watendaji na madiwani kuhusu diplomasia ya uchumi na utatuzi wa migogoro.

Mheshimiwa Peter alisema mafunzo haya kwa waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Temeke yaliandaliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke na yaliyafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Temeke, Jijini Dar es Salaam.

“Mafunzo kuhusu Utatuzi wa Migogoro katika ngazi ya Halmashauri na Manispaa na Mchango wa Serikali za Mitaa katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi ni muhimu sana kwetu sisi, tunaamini tutakuwa na utambuzi wa maarifa ambayo yatatuwezesha kutekeleza majukumu yetu kwa weledi” alisema Mheshimiwa Peter.


Naibu Meya alitoa wito kuwa mafunzo haya ni vizuri yakatolewa kwa watendaji wa Halmashauri na Kata ili waweze kushirikiana kwa pamoja katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.

Kwa upande wake, Dkt. Jason Nkyabonaki, Mkuu wa Taaluma aliyemuwakilisha Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Dkt. Salim Ahmed Salim, Dkt. Felix Wandwe, ndc alisema mafunzo haya ni muhimu kwa Madiwani hasa tukitambua kuwa nyakati hizi wasomi wameelekeza kuwa katika karne ya 21 ujinga si kutojua kusoma na kuandika bali mjinga ni yule ambaye hawezi kujifunza.

“Tumejifunza misingi ya Uongozi, dhana ya Diplomasia ya Uchumi na namna ya kutatua migogoro. Hatuwezi kutatua migogoro katika mazingira ya wenye njaa. 

Kupitia mafunzo haya waheshimiwa Madiwani naomba tuzidi kuwa pamoja, tunahitaji namna bora ya kukaa pamoja na tambueni kuwa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim ni Kituo bora na salama cha kujifunzia. Nachukua fursa hii, kwa niaba ya Uongozi wa Kituo kuwaomba waheshimiwa Madiwani  mlioko hapa kuja CFR, waleteni pia ndugu, jamaa na vijana wenu, Kituo kinatoa kozi mbalimbali tunawaalika mje kuongeza maarifa ” alisema Dkt. Nkyabonaki.


“Ninaamini waheshimiwa Madiwani baada ya mafunzo haya mtakuwa mabalozi wazuri wa kukisemea Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kuwa ni kituo bora kinachotoa programu za mafunzo kulingana na mahitaji ya sasa na kinatoa wahitimu wenye weledi na mahiri wanaotambulika kitaifa na kimataifa” alifafanua Dkt. Nkyabonaki.

Akizungumzia kuhusu mafunzo yaliyotolewa kwa madiwani, mratibu wa mafunzo Bibi Janeth Malleo alisema mafunzo haya kwa waheshimiwa Madiwani na Watendaji wa Manispaa ya Temeke yamefanyika ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Kituo kwa kushirikiana na Uongozi wa Halmashauri ya Temeke ili kuwezesha Madiwani kutekeleza kazi zao vyema za kusimamia Halmashauri lakini pia kuwawezesha wananchi vyema katika Kata zao.

Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kimelenga kutoa mafunzo ya utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi kwa watendaji wa Serikali na wadau kutoka Sekta binafsi. 


Hii itasaidia utekelezaji mzuri wa Diplomasia kwa wadau husika ikiwa ni pamoja na Sekta binafsi, Wajasiriamali wa kati na wadogo katika kuchangamkia fursa za masoko nje ya nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post