FCC KUTUMIA AKILI MNEMBA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI

 

Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.

Kukua kwa Teknolojia katika Sekta ya TEHAMA na uwepo wa akili mnemba (IA), kutasaidia kuongeza tija na ushindani wa Biashara huku elimu zaidi ikihitajika kwa wadau na wananchi kuhusu Teknolojia hiyo.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 30,2024 Jijini Dar es Salaam, na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), William Erio, katika kongamano la siku moja la kujadili matumizi ya akili mnemba yanayozingatia haki na uwajibikaji kwa mlaji.

Erio amesema kuwa hivi sasa Biashara nyingi zinafanywa kwa njia ya mifumo ya kimtandao na huduma nyingi zinatolewa na akili mnemba, hivyo FCC inaangalia jinsi ambavyo inaweza kutumia Teknolojia hiyo kumlinda mlaji kwa mujibu wa kanuni na Sheria

“Tunaangalia na kuzingatia hii akili mnemba inaangalia haki katika upangaji bei, mfano unapokata tiketi ya ndege bei unayopata ni sahihi na huduma unazopata” amesisitiza.

Aidha, ameeleza kuwa wataangalia vikwazo mbalimbali vilivyopo vya kisheria ili hatua stahiki zichukuliwe na kuhakikisha matumizi ya akili mnemba yanatambulika kisheria.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya FCC, Dk Agrey Mlimuka amesema kuwa azma hiyo itakuwa na maana pale mifumo ya kiteknolojia itazingatia uwajibikaji ,tija, ,haki na usawa kwa kuwekewa mifumo thabiti ya usimamizi na udhibiti.

Ameongeza kuwa kazi iliyopo sasa ni kuboresha na kurahisisha utoaji wa huduma zenye ubora kwa walaji kwa kutumia teknolojia kama nyenzo muhimu kwa ustawi wa walaji na uchumi kwa ujumla.

“Sote tunashauku ya kuboresha na kurahisisha utoaji huduma bora kwa walaji, kutumia teknolojia kama nyenzo muhimu kwa ustawi wa maslahi ya walaji na uchumi kwa ujumla" ameeleza" Dkt. Mlimuka.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani, Jaji Salma Maghimbi amasema lazima wawe sehemu muhimu kwa kuangalia teknolojia hiyo ili kumlinda mlaji kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.

kongamano hilo limejumuisha wadau na watalaam mbalimbali wakiwemo TEHEMA, Vyuo Vikuu, Taasisi za Utafiti , Afya, Sera na Sheria, pamoja na wafanyabiashara kutoka Sekta Binafsi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post