DAWASA YAZIJENGEA UWEZO KAMATI ZA MIRADI KISARAWE

 


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeendesha mafunzo kwa Kamati ya kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi wakati wa utekelezaji wa miradi ya majisafi iliyopo Wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani.

Akizungumza na wanakamati Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mhe. Fatma Nyangasa ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati kwa ngazi ya Wilaya ameeleza kuwa mafunzo haya ni muhimu kwani yanawafanya kuwa na uelewa wa pamoja kipindi cha utekelezaji wa miradi na hatua za kufuata kutatua changamoto.

"Kamati hizi zinaokoa muda wa wanachi pindi linapotokea jambo kipindi cha mradi, niwaahidi DAWASA nitasimamia vyema kamati hii na kutoa ushirikiano mkubwa ili nia ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani iweze kutimia.

Mhe. Nyangasa ameongeza kwa kuwataka DAWASA kuandaa ziara maalumu ya kamati ya kushughulikia malalamiko wakati wa utekelezaji wa miradi Wilaya ya Kisarawe kufika katika miradi inayotekelezwa Dar es salaam ya Kusini pamoja na ule wa ujenzi wa mitambo midogo ya kuchakata majitaka.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mazingira DAWASA, Mhandisi Modesta Mushi ameeleza kuwa ni muhimu kuunda na kuzipa elimu ya mara kwa mara kamati hizi kwani ni msaada mkubwa katika kuhakikisha miradi inatekelezwa na kukamilika kwa wakati uliopangwa.

Wilaya ya Kisarawe ni wanufaika wa miradi inayotekelezwa na DAWASA katika Kata ya Kiluvya, ikiwa ni mradi wa ujenzi wa mitambo midogo ya kuchakata majitaka (FSTP) pamoja na mradi wa uboreshaji huduma ya maji Dar es salaam ya Kusini ambayo kwa pamoja itanufaisha zaidi ya wakazi 3,500. 
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post