WATOTO WATATU WAFARIKI WAKIOGELEA KWENYE BWAWA TINDE


Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Watato watatu wamefariki dunia baada ya kutumbukia katika bwawa lililopo eneo la Ngaka kijiji cha Nyambuhi kata ya Tinde Wilayani Shinyanga.

Tukio hilo limetokea leo May 16, 2024 majira saa 4 asubuhi katika kijiji cha Nyambuhi ambapo watoto hao wakiwemo wawili wa familia moja ambao ni Salama Said darasa la sita, Amina Faraji  na Prisca Mabula waliokuwa wakisoma darasa la nne katika shule ya msingi Tinde B ambapo walifika katika bwawa hilo kwa lengo la kuogelea ndipo walizama na kupoteza maisha huku mmoja kati ya wanne akisalia.

Akisimulia tukio hilo bibi wa watoto hao wawili amesema majira ya asubuhi walitoka nyumbani wakiaga kuwa wanaelekea shuleni muda mfupi baadae alipokea taarifa ya kuzama kwa wajukuu wake wawili.

Baadhi ya wakazi wa eneo hilo akiwemo Maganga Malekela amesema hilo ni tukio la tatu kutokea kwenye bwawa hilo huku wakiiomba serikali kuchukua hatua ili kupunguza vifo vinavyosababishwa na watu kuzama kwenye bwawa hilo.

Kaimu kamanda wa Jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoa wa Shinyanga  Ramadhan Kamo amethibitisha kuopolewa kwa miili ya watoto hao na kuwasihi wakazi wa eneo hilo kuwa waangalifu kwa watoto na kubainisha kuwa wamefanikiwa kuopoa miili yote mitatu iliyokuwa imezama.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post