RAIS MWINYI AVUTIWA NA UTENDAJI WA BENKI YA CRDB KATIKA KUTENGENEZA FAIDA


Arusha 17 Mei 2024 - Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kutengeneza faida kubwa inayoiwezesha benki hiyo kutoa gawio kwa wanahisa wake kutokana na uwekezaji wao ndani ya benki hiyo.

Rais Mwinyi alitoa pongezi hizo wakati akifungua semina ya uwekezaji na elimu ya fedha iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wanahisa wake na Watanzania kuelekea Mkutano Mkuu wa 29 wa Wanahisa utakaofanyika Jumamosi Mei 18, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
“Nadhani sitakuwa nimekosea nikisema ongezeko la faida baada ya kodi ambayo Benki yetu ya CRDB imepata mwaka jana kufikia Sh bilioni 424 kulinganisha na Sh bilioni 351 mwaka 2022, ni ukuaji mkubwa wa faida kupata kutokea,” alisema Rais Mwinyi.

Alisema kuwa Benki ya CRDB imeendelea kudhihirisha kivitendo kuwa “Benki kiongozi” nchini kwani kila mwaka imekuwa ikiendelea kutoa faida ya uwekezaji kwa wanahisa wake huku akizitaka taasisi nyengine za umma na binafsi kuiga mfano.

“Nimefurahishwa pia kusikia mwaka huu Bodi ya Wakurugenzi imekuja na pendekezo la ongezeko la asilimia 11 ya gawio kwa hisa. Wanahisa wa Benki ya CRDB mnastahili kutembea kifua mbele kwa ongezeko hili,” aliongezea Rais Mwinyi.

Rais Mwinyi pia aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa semina ya elimu ya fedha na uwekezaji kwa ajili ya wanahisa wake na Watanzania huku akibainisha kuwa umahiri wa masuala ya fedha wa wananchi ni moja ya msingi muhimu wa maendeleo ya watu wa taifa lolote duniani.

“Niwapongeze Benki ya CRDB kwa kuongoza katika utoaji wa elimu ya masuala ya fedha kwa Watanzania. Siku chache zilizopita, mliandaa semina mliyoiita CRDB Bank Uwekezaji Day, mimi niliifuatilia kupitia televisheni,” Rais Mwinyi alisema huku akiitaka benki hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuongeza ujumuishi wa kifedha.

Katika hotuba yake, Rais Mwinyi pia alisisitiza umuhimu wa sekta ya fedha katika maendeleo ya taifa, akitambua mchango mkubwa wa Benki ya CRDB katika kuimarisha uchumi wa Tanzania, bara na Zanzibar. Alieleza jinsi Benki ya CRDB imekuwa mshirika muhimu katika kuendeleza dhana ya Uchumi wa Buluu, kupitia programu kama vile 'INUKA na Uchumi wa Buluu', ambazo zimechangia sana katika sekta za utalii, kilimo, ufugaji, uvuvi, mafuta, biashara, na ujasiriamali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay alisema benki hiyo ikiwa benki ya kizalendo inayomilikiwa na Watanzania kwa zaidi ya asilimia 80, inajivunia kuendelea kukuza thamani ya uwekezaji wa wanahisa wake ikiwamo Serikali ambayo inamiliki asilimia 36 ya hisa katika benki hiyo.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni mwanahisa wa Benki hiyo kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Zanzibar (ZSSF). Dkt. Laay amewakaribisha Watanzania wengine kuwekeza ndani ya Benki ya CRDB ili nawao waanze kunufaika na gawio nono ambalo limekuwa likitolewa na Benki hiyo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela alisema malengo ya semina hiyo ni kuwajengea uwezo Wanahisa wao pamoja na Watanzania wengine ili kuwajengea uwajibikaji wa kifedha na kuongeza ushiriki katika fursa za uwekezaji hususan katika soko la hisa la Da es Salaam.
“Kwa kutoa elimu hii Wanahisa wetu pia wanapata kufahamu zaidi faida za kuwekeza katika Benki yao ya CRDB, hivyo basi kuongeza uwekezaji na kupata faida nono zaidi, lakini pia kuwahamasisha na Watanzania wengine pia kuwekeza katika hisa hususan za Benki ya CRDB na kuanza kupata gawio,” aliongezea Nsekela.

Aidha, Nsekela alimshukuru Rais Mwinyi kwa ushirikiano wa kimkakati na mazingira mazuri ya biashara ambayo ndio chachu ya utendaji mzuri wa benki hiyo. Kadhalika, alimhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa Benki ya CRDB itaendelea kuwezesha uchumi wa Zanzibar kwa kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo hususan katika kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa za Uchumi wa Buluu.

Katika semina hiyo, mada mbalimbali zilijadiliwa, ikiwa ni pamoja na Ujumuishi wa Kifedha, Uwekezaji katika Hisa, Hatifungani ya Kijani ya Benki ya CRDB, Wosia na Mirathi, pamoja na Kinga dhidi ya Majanga.
Semina ya Wanahisa iliyofanyika leo ni sehemu ya maandalizi kuelekea Mkutano Mkuu wa 29 wa Benki ya CRDB utakaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) na kupitia Mtandao. Mkutano huo unatarajiwa kuaanza saa 3 asubuhi, ambapo watu wa mtandaoni wataweza kujiunga kupitia link https://escrowagm.com/crdb/login.aspx au kupitia SimBanking App.

Benki ya CRDB imeweka muongozo wa jinsi ya kushiriki mkutano mkuu kwa njia ya mtandao kupitia tovuti yake ya www.crdbbank.co.tz, mitandao yetu ya kijamii ya Instagram, twitter, lakini pia maelekezo yametumwa kwa ujumbe mfupi kwa Wanahisa.
Sehemu ya Wanahisa wakiwa katika Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB ambayo imefanyika leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) kuelekea Mkutano Mkuu wa Benki hiyo utakaofanyika hapo kesho.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda akizungumza katika Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB ambayo imefanyika leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) kuelekea Mkutano Mkuu wa Benki hiyo utakaofanyika hapo kesho.
Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar, Saada Mkuya Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB ambayo imefanyika leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) kuelekea Mkutano Mkuu wa Benki hiyo utakaofanyika hapo kesho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post