BMM KWA KUSHIRIKIANA NA BYABATO WAWAGUSA WAATHIRIKA WA MAFURIKO BUKOBA

 
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Bukoba mjini Mhandisi Pasaka Bakari akikabidhi msaada uliotolewa na wadau wa group la Bukoba mjini mpya kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Bukoba mjini Adv Stephen Byabato
Jamila Emily ambaye ni mmoja wa wadau wa group la Bukoba mjini mpya akikabidhi msaada wa chakula kwa muathirika wa mafuriko   
Baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na mvua
Wadau wa group la Whatsapp la Bukoba mjini mpya baada ya kufika ofisi ya kata ya Hamgembe kutoa msaada kwa waathirika wa mafuriko
Wadau wa Group la Whatsapp  la Bukoba Mjini Mpya ambao ni Asimwe na Fatna wakiwa wamebeba mahitaji kwa ajili ya waathirika wa Mafuriko



Na Mariam Kagenda_Kagera 

 Wadau wa group la Whatsapp la  Bukoba mjini mpya kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Bukoba mjini Adv Stephen Byabato wametembelea na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea usiku wa kuamkia  Mei 9 mwaka huu katika kata saba za  Manispaa ya Bukoba.

Wadau hao wamefika katika kata hizo  ambazo zimeathiriwa na mafuriko hayo na kutoa vitu mbalimbali ikiwemo Mchele,Unga,Mafuta, Sabuni,Maharage na nguo kwa ajili ya kuwasaidia waathirika hao wa mafuriko kupata mahitaji hayo muhimu ambapo kila kata kaya 15 zimepatiwa msaada huo.

Baadhi ya wadau wa group hilo Jamila Emily,Erick Bashabi ,Sharifa Karwani ,Asimwe na Husna wamesema kuwa waliopata mafuriko wanahitaji msaada kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo hivyo kwa umoja wao waliona ni vyema kuungana kwa pamoja  kuchangishana kama wana group ili kuwasaidia waanga hao .

Wameongeza kuwa group hilo limekuwa na utaratibu wa kushirikiana kwa pamoja  katika mambo mbalimbali yanayoigusa jamiii hivyo hata waanga wa mafuriko yaliyotokea manispaa ya Bukoba ni vyema wakasaidiwa .

Kwa upande wake katibu wa Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini Mhandisi Pasaka Bakari amesema kuwa baada ya mafuriko kutokea ofisi ya mbunge ilifika kwa waathirika wa mafuriko katika kata zote 7 zilizoathirika na mafuriko hayo  ili kuona athari zilizotokana na mafuriko hayo ambapo  amewashukuru  wadau   mbalimbali wa maendeleo katika Manispaa ya Bukoba wanaoendelea kuwasaidia waathirika wa mafuriko na kuwaomba wengine kuendelea  kujitokeza  kuwasaidia.

Amesema kuwa Mbunge wa Jimbo  la Bukoba mjini  Adv Stephen Byabato ataendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuona namna ya kuwasaidia waathirika wa mafuriko.

Kwa upande wake Afisa tawala wilaya ya Bukoba mjini akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Bukoba Ajesy Katumwa amewashukuru wadau wa group la Bukoba mjini Mpya kwa ushirikiano wao na kuona umuhimu wa kutoa misaada hiyo kupitia michango yao.

Bwana Katumwa amesema kuwa mafuriko hayo yamesababisha uharibifu wa miundombinu mbalimbali ikiwemo makazi ya wananchi kujaa maji,barabara kufungwa kwa muda katika baadhi ya maeneo pamoja na wananchi kuharibikiwa na mali zao.

Nao wananchi waliopatiwa msaada huo wameshukuru wadau wa Group la Bukoba Mjini Mpya pamoja na Mbunge wa Jimbo la Bukoba mjini   kwa msaada walioutoa kwani mvua hizo zilisomba vyakula pamoja na vitu vingine  na maji yamejaa kwenye nyumba zao hivyo  kuwahimiza wadau wengine kuendelea kutoa msaada kwa sababu wahitaji ni wengi walioathiriwa na mafuriko hayo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post