WAKULIMA WA SKIMU YA TITYE WAOMBA KUBORESHEWA MIUNDOMBINU


Wakulima wa mpunga na wataalamu kutoka taasisi ya TARI, ANPI na viongozi wa serikali mkoani Kigoma wakikagua mashamba ya mpunga na miundombinu ya umwagiliaji skimu ya Titye kwaajili ya kutambua mafanikio na changamoto zilizopo ili kufanya uboreshaji
Adela Madyane -Kigoma

Wakulima 800 wa zao la mpunga katika skimu ya umwagiliaji ya Titye iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma wameiomba serikali kuboresha miundombinu ya mto Ruchugi ambao ndio unaotumika kwa umwagiliaji katika mashamba ya wakulima hao.

Akitoa ombi hilo mwenyekiti wa skimu hiyo Daud Mubingo alisema anaomba mifereji ya umwagiliaji kutoka kwenye mto huo ijengewe hadi mwisho  ili kurahisisha zoezi la umwagiliaji kwa baadhi ya mashamba ambayo yamekuwa hayapati maji.


“Wakati mwingine baadhi ya mashamba yanakuwa na maji mengi, mengine yanakuwa na maji kidogo na mengine yanakosa maji kabisa, tunaiyomba serikali iturekebishie mifereji hiyo kwakuwa tuanachangia kwenye tume ya umwagiliaji ya taifa mfano kwa msimu wa 2022/2023 tumelipa ada ya shilingi milioni sita” Alisema Mubingo.


Akizungumzia kuhusu mafanikio ya skimu hiyo yenye hekta zaidi ya 700 Mubingo alisema kwa kipindi cha msimu wa pili wa kilimo hicho, 2023/2024 wamefanikiwa kuongeza uzalishaji kutoka gunia tano za mpunga kwenye shamba la ukubwa wa ekari moja hadi kufikia gunia 31.5 jambo ambalo linatia motisha kwa wakulima wengi kujiingiza katika kilimo hicho.


Alisema hatua hiyo ya uzalishaji imetokana na kuzingatia maelekezo ya kilimo chenye tija kutoka kwa wataalamu wa kilimo wa Taasisi ya Utafiti ya Kilimo Tanzania (TARI) ofisi za Kihinga Kigoma ambao wamekuwa washikirikiana na wakulima katika kila hatua ya uzalishaji kupitia mashamba darasa.


Mwenyekiti ametoa angalizo kwa wakulima watakaolima bila kufuata kanuni bora za kilimo ikiwemo kulima bila kukata mstaru kwa msimu wa 2024/2025 watatakiwa kulipa faini ya shilingi elfu 50,000/= kwa wakulima wa skimu ya Titye,  hii ikiwa ni hamasa kuwa kila mkulima kufanya vizuri na  kufanikiwa.


Sambamba na kuboresha miundombinu ya mifereji Felix Lukeba mwenyekiti wa kijiji cha Titye aliomba pia watengenezewe barabara zinazounganisha madaraja kwaajili ya kupitisha mazao kwani wao kama wakulima walijienga madaraja yaliyokuwa hayapitiki ili kurahisisha usafirishaji.


“Tulitumia nguvu kubwa kujenga madaraja ili kurahisisha usafirishaji, bahati mbaya mwaka huu mvua zimekuwa nyingi, barabara zimeharibika, tunaomba serikali itusaidie kwenye maeneo tuliyojenga madaraja watuunganishe na barabara ili tuweze kupita kwakuwa tunazunguka umbali mrefu kutafuta barabara inayopitika na hivyo kuongeza gharama za usafirishaji kwa mkulima”, alisema Lukeba.


Naye Eliazar Mizigiro diwani wa kata ya hiyo alisema ni muhimu kwa taaisisi ya TARI kutoa mbegu za kisasa za kilimo cha mpunga zinazohitajika katika kuongeza uzalishaji sambamba na mbolea zinazotosheleza mahitaji ili kufikia azma ya serikali ya kumtoa mkulima kwenye kilimo duni na kumuingiza kwenye kilimo chenye tija.

“Nia ya mabadiliko tunayo kwakuwa tumejionea kwa macho namna ambavyo uzalishaji kwa kutumia kilimo cha kisasa unavyomsaidia mkulima kutoka kwenye umaskini, naomba serikali kupitia TARI ituletee mbegu na mbolea kwa wakati, na maboresho ya miundombinu mingine ifanyiwe kazi kwa wakati kwaajili ya ustawi wa mkulima na taifa kwa ujumla”,alisema Mizigiro.


Mizigiro aliwaomba wataalam wa kilimo kutoka ngazi ya mkoa na TARI Kihinga kufika katika mashamba yao mara kwa mara ili kutatua changamoto za uzalishaji zinazojitokeza kama ilivyotokea kwenye mifereji ya umwagiliaji kupasuka na kukaa muda mrefu bila kupata suluhu ya kudumu.

 
Mkulima Nicholous Kibadi aliwataka wakulima wenzake kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wa kilimo ,kwa sababu ya manufaa yatokanayo na ushauri huo kwani kwa upande wake amenufaika na kuongeza kipato, kusomesha watoto katika shule za watu binafsi pamoja na kubadili chakula kitu ambacho kilikuwa kigumu kwake kabla ya kuongeza uzalishaji.

Kwa upande wa mhandisi wa kilimo mkoani Kigoma Bathromeo Moris alisema serikali inaendelea kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji na kwamba fedha za ukarabati wa miundombinu ya mifereji zitakuja kupitia tume ya umwagiliaji huku akiwasihi kuzingatia usafi wa mifereji hiyo ili kuifanya kuwa endelevu. 


Akizungumza mkurugenzi wa TARI Kihinga mkoa wa Kigoma Filson Kagimbo alisema kilimo cha umwagiliji cha zao la mpunga mkoani humo ni matokeo ya mradi wa mapinduzi ya kilimo kupitia urutubishaji wa mazao ya nafaka Afrika (NUTCAT)  kwa kushirikiana na Taasisi ya kurutubisha mimea Africa (ANPI) unaotekelezwa katika nchi 10 za Afrika katika mazao manne yakiwemo mahindi, mpunga na ngano kwa muda wa miaka mitatu kuanzia 2022/2024.

Kagimbo alisema mradi huo kwa Tanzania unaotekelezwa mkoani Kigoma katika wilaya za Kakonko, Kasulu na Kigoma ambapo mpaka sasa mradi huo umekuwa na tija kwa wakulima kuongeza uzalishaji.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Katibu tawala wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Theresia Mtewele alisema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, ongezeko la matumizi ya ardhi na ongezeko la watu linasababisha kupungua kwa rutuba kwenye ardhi na hivyo kupunguza uzalishaji hivyo nchi imejiwekea mikakati ya kuongeza uzalishaji


“Lengo la taifa kupitia ajenda ya 1030 ni kujitosheleza kwa chakula na kuwa ghala la chakula la Afrika ifikapo 2030 hivyo serikali imejikita katika kufanya utafiti, uboreshaji na uendeshaji wa miundombinu ya umwagiliaji upatikanaji rahisi wa pembejeo pamoja na huduma za ugani na tunaona namna ambavyo uzalishaji unaongezeka kufuatia mikakati hiyo", alisema Mtewele.


Alisema kwa takwimu za uzalishaji wa zao la mpunga kwa mwaka 2021 zao  hilo lilizalishwa mpaka kufikia tani milioni 2.6 na kwamba mpaka sasa zao hilo limezalishwa kwa zaidi ya tani milioni 3 kwa mwaka jambo ambalo linaonesha namna taifa  lilivyifanikiwa katika usalama wa chakula.

Hata hivyo Mtewele alisema changamoto za mifereji na barabara zilizotolewa na wakulima zitafanyiwa kazi kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa kilimo na kwamba watawasiliana na mamlaka husika kama wakala wa barabara za mjini na vijijini (TARURA) ili waweze kuunganisha barabara na madaraja yaliyojengwa na wananchi.


Metewele aliwataka wakulima kuendelea kukitunza chanzo cha maji ya mto Ruchugi ili watu wengi wanufaike na matumizi ya maji katika kilimo cha umwagiliji na kwaajili ya mustakabali wa kizazi cha sasa na kijacho.


Bajeti ya kilimo kwa mwaka 2023/2024 imeongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 970.8 kutoka shilingi bilioni 954 kwa mwaka 2022/2023 ili  kuhakikisha lengo la taifa kupitia ajenda ya 1030 la kujitosheleza kwa chakula na kuwa ghala la chakula la Afrika ifikapo 2030 linafikwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post