WMAs ZATAKIWA KUWA NA MATUMIZI SAHIHI YA FEDHA
 Na mwandishi wetu, DODOMA

Serikali imewataka viongozi wa Jumuiya za Hifadhi Wanyamapori (WMAs) kuzingatia matumizi sahihi ya fedha  ili kuwanufaisha wananchi wa vijiji wanachama   pia kuzingatia mikataba inayoingiwa na WMAs hizo  kwa maslahi ya Taifa.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ametoa kauli hiyo  leo Aprili 8,2024 Jijini Dodoma wakati wakati wa kikao cha viongozi wa Jumuiya hizo pamoja  na baadhi ya maofisa wanyamapori wa wilaya kuhusu changamoto za usimamizi wa maeneo ya WMAs nchini.

Amesema rasilimali fedha ni lazima  zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuendeleza miradi ya maendeleo ya vijiji kwa kuwashirikisha wananchi wa vijiji hivyo. 

 “Ni lazima muweke mkazo katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na uwazi na matumizi sahihi ya fedha pamoja na  utoaji wa taarifa kwa wanufaika kwenye vijiji husika, msipofanya hivyo uongozi utageuka shubiri mtakapofanyiwa ukaguzi” Mhe. Kairuki alisisitiza.

Amesema kuwa katika kipindi cha Mwaka wa fedha  2022/2023 Serikali imetoa mgao wa takribani bilioni 9.6 ambazo Serikali  inaamini zimetumika kwa mujibu wa Kanuni za WMAs ambazo zinaelekeza kuwa sehemu ya fedha hizo zitumike kutekeleza miradi ya maendeleo ya vijiji. 

Amesema kupitia kanuni hizo za uanzishaji na uendelezaji wa maeneo ya hifadhi kwa sasa kuna jumla ya WMAs 22 zilizodhinishwa na kupata haki ya matumizi ya rasilimali za wanyamapori lakini kuna nyingine 16 ambazo ziko kwenye mchakato wa kuanzishwa.

Aidha, ametumia fursa hiyo kuzishukuru WMAs kwa mchango wao katika kusaidia  kukuza uchumi kwa mtu mmoja mmoja na katika jamii  pamoja na kusaidia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika jamii na vijiji wanachama.

“Hii imejidhirishisha katika Sekta ya uwindaji wa Kitalii na utalii wa picha ambapo tumeshuhudia umekuwa chachu ya uchumi  kwa vijiji wanachama ambao wanaunda jumuiya zetu” Mhe. Kairuki amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wadau wa uhifadhi imeendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha Jumuiya zinaendelea kuimarika ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo viongozi wa WMAs kwa lengo la kuimarisha utawala na usimamizi wa maeneo hayo na kuwezesha mafunzo kwa Askari wa Wanyamapori wa Vijiji (VGS) ambapo takribani VGS 540 wamepata mafunzo katika Chuo cha Wanyamapori Likuyuseka – Maganga.

Pia amesema Serikali imewezesha upatikanaji wa vitendea kazi ikiwemo magari ya doria kwa baadhi ya Jumuiya kama Mbarangandu na Nalika, Vilevile, Jumuiya zimewezeshwa vifaa vya uwandani kama vile mahema, GPS, kamera, sare za Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) na vifaa vya ofisini kama kompyuta katika Jumuiya za MBOMIPA, WAGA na UMEMARUWA.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamishna CP Benedict Wakulyamba, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dkt. Fortunata Msoffe ,Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA,wawakilishi wa Makamishna Uhifadhi wa TANAPA, NCAA na TFS, Wakuu wa Idara na Taasisi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Maafisa Wanyamapori wa Wilaya, Wadau wa Wizara ya Maliasili na Utalii na  Viongozi wa Jumuiya za Wanyamapori.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post