WANAWAKE WAHAMASISHWA KUSHIRIKI MAANDAMANO YA CHADEMA BUKOBA


Na Mbuke Shilagi Bukoba.

Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo BAWACHA Mkoa wa Kagera amekutana na Baraza la Wanawake wa Chama hicho Wilaya ya Bukoba Mjini ili kuzungumza nao katika ushiriki wa zoezi la maandamano ya amani yatakayofanyika mnamo tarehe 22 April 2024 katika Wilaya ya Bukoba Mjini.

Akizungumza katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa mexiko hotel uliopo Kata ya Kashai Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera April 17,2024 Mwenyekiti wa BAWACHA Mkoa wa Kagera Bi. Magreth Domisian Kyai amesema kuwa maandamano ni suala la kila mmoja hivyo wanawake kwa pamoja wajitokeze ili kudai marekebisho ya katiba mpya.

Bi Magreth ameongeza kuwa vikao kazi vitaendelea katika majimbo yote ndani ya Mkoa wa Kagera ikiwa ni kuendelea kuwahamasisha wanawake kujitokeza kushiriki maandamano ya amani na kwamba kwa namna ya pekee katika Kanda ya Ziwa Victoria  yameanzia Kagera Bukoba Mjini hivyo akina mama wajitokeze maana wao ni jeshi kubwa.

Sambamba na hayo katika kikao kazi wameweza kuzungumzia masuala mbalimbali ya kichama ikiwa ni pamoja na ujenzi wa ofisi lakini pia kujengeana uzoefu wa kila mwanamke wa BAWACHA kujiamini kisiasa na kiuchumi ili kuhakikisha katika chaguzi za serikali za mitaa na chaguzi za serikali kuu wanajitokeza na kushika nyadhifa mbalimbali.

Aidha kikao kazi hicho kimehudhuliwa na viongozi mbalimbali ngazi ya Wilaya,Mkoa,Kanda ya Ziwa Victoria mpka Taifa na kwapamoja wamesema kuwa lengo la maandamano ni kupaza sauti ambazo hazisikiki hivyo wataendelea na maandamano Kanda kwa Kanda, Mkoa kwa Mkoa, Wilaya kwa Wilaya, Kata kwa Kata mpaka Serikali itakaposikia na kuyafanyia kazi yote ambayo hayako sawa ikiwa ni pamoja na katiba mpya.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post