GILITU AFUNGA MASHINDANO YA UMISETA KANDA YA MWASELE KWA KISHINDO, AMWAGA ZAWADI KWA WASHINDI



Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Lubaga Gilitu Makula amewashauri walimu wa shule nne za kanda ya Mwasele kudumisha na kuendeleza michezo kwa kuwa michezo ni afya na ni ajira kwa vijana.

Ushauri huo ameutoa leo tarehe 24.04.2024 wakati wakihitimisha mashindano ya umiseta kanda ya Mwasele yenye shule za sekondari nne ambazo ni Lubaga, Mwasele, Mwangulumbi na Hope Extended katika shule ya Sekondari Lubaga.

Makula akizungumza na walimu, wafanyakazi na wanafunzi wa shule zote nne, amewasihi walimu kudumisha na kuendeleza michezo maana michezo ni afya, na ni ajira na michezo hudumisha mahusiano.

Pia Makula ambaye ni mwenyekiti wa bodi hiyo amewapatia chakula walimu, wanafunzi, na wageni zaidi ya watu 2000 na ametoa zawadi za fedha taslimu sh 500,000. kwa washindi wote ambao ni wachezaji bora, wafungaji bora na wanariadha walioshinda mbio zote.

Katika Shule ya Mwasele Sekondari amewazawadia mipira mitatu kwa kuwa ni shule iliyoshinda mpira wa miguu wavulana na netball, pia shule ya Mwangulumbi sekondari
amewazawadia mipira 3 kwa kushinda mpira wa miguu wasichana.

Aidha wakuu wa shule wa Lubaga Mwasele, Hope na Mwangulumbi walimzawadia mwenyekiti huyo picha kubwa yenye maneno ya shukrani.

Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Lubaga mwalimu Hamisa Boniphace kwa niaba ya wakuu wa shule wa kanda ya Mwasele alimshukuru Mwenyekiti Makula kwa kuwa na moyo wa kujitoa kwa jamii hasa katika sekta ya elimu na michezo.

"Ndugu mgeni rasmi na mwenyekiti wetu bodi ya shule ya Lubaga tunakupongeza kwa dhati kwa namna ambayo umekuwa ukijitoa, ikimbukwe na wewe mwenyewe ulituwezesha magori ya mpira wa miguu na wavu, magori na wavu wa volleyball pamoja na magoli ya mchezo wa pete,"amesema Hamisa.

" Pia tunakushukuru kwa kutupatia jezi za kutosha na mipira mitano, na hii imekuwa ndiyo sababu ya shule yetu ya Lubaga kuchaguliwa kuwa kituo cha michezo katika kanda yetu hii ya Mwasele., hivyo tunakushukuru sana tena sana kwa kujitoa kwako,"ameongeza.

Naye mwakilishi wa Afisa elimu Mwalimu Chibugu Mugini alimshukuru Makula kwa kuwa chachu ya michezo na taaluma, na kutoa chakula na zawadi kwa washindi, hivuo michezo ya umiseta imefungwa leo katika ngazi za kanda.
























































Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post