POLISI SHINYANGA WAKAMATA SIMU ZA WIZI, MAFUTA YA DIZELI, MATAIRI YA GARI

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limekamata mafuta ya dizeli lita 320, vipande 250 vya nondo,  Simu za wizi, Nyaya na matairi ya gari baada ya kufanya doria, misako na Operesheni mbalimbali.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Aprili 17,2024 Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Kennedy Mgani amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linaendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa kushirikiana na Jamii katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu kwa kufanya doria, misako pamoja na operesheni mbalimbali katika kipindi cha wiki tatu kuanzia Machi 28, 2024 mpaka Aprili 16, 2024.

"Katika kipindi hicho, Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata mafuta ya dizeli lita 320, Vipande 250 vya nondo, Nyaya mbalimbali, matairi 05 ya gari, Injini 01 ya Pikipiki, Betri 06 za gari, Mashine 01 ya kukatia miti (chain saw), mitambo 04 ya kutengeneza pombe ya moshi (gongo), pombe ya moshi lita 13, bhangi kete 33, Simu 05, Pikipiki 04, Mashine 01 ya bonanza, Redio 02, mtungi 01 wa gas, TV 01 pamoja na vifaa mbalimbali vya kupigia ramli chonganishi", amesema Kaimu Kamanda Mgani.

"Jumla ya kesi 09 zimepata mafanikio ambapo kesi 01 ya kubaka ambapo mshtakiwa alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, kesi 02 kupatikana na bhangi washtakiwa 02 walihukumiwa kifungo cha miaka miwili mpaka mitatu jela, kesi 01 kuvunja nyumba usiku na kuiba mshtakiwa 01 alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, kesi 01 kuharibu mali mshtakiwa alihukumiwa kifungo cha mwaka 01 jela, kesi 03 za wizi washtakiwa 03 walihukumiwa kifungo cha miezi06 jela na kesi 01 kuingia kwa jinai mshtakiwa alihukumiwa kifungo cha miezi 04 jela",ameongeza.


Katika hatua nyingine amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kikosi cha Usalama barabarani limefanikiwa kukamata jumla ya makosa 3,771 ambapo makosa ya magari ni 2,836 na makosa ya bajaji na pikipiki ni 935 wahusika waliwajibishwa kwa kulipa faini za papo kwa hapo.

"Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linawashukuru Wananchi kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha Usalama wa Mkoa wa Shinyanga unakuwa shwari, Pia linatoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutii na kufuata sheria na halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayekiuka sheria za nchi",amesema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post