RAIS SAMIA AWAONYA WAFANYABIASHARA WANAOKWEPA KODI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wageni mbalimbali pamoja na Waumini wa Dini ya Kiislamu kwenye Baraza la Eid El Fitr ambalo Kitaifa limefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam tarehe 10 Aprili, 2024.

*Asema serikali yake ilikataa kodi za dhuluma, lakini wafanyabiashara wamegeuka na kuidhulumu serikali kodi

Aprili 11, 2024

Na Mwandishi Wetu

Rais Samia Suluhu Hassan amewaonya wafanyabiashara wanaokwepa kodi nchini, huku akisema kuwa dhuluma hiyo inachelewesha maendeleo ya nchi.


Rais amesema kuwa licha ya makusanyo ya kodi kuongezeka ndani ya miaka mitatu iliyopita, bado kuna wafanyabiashara nchini wanakwepa kodi.


Samia amesisitiza kuwa Serikali yake ya Awamu ya 6 iliachana na mfumo wa kukusanya kodi kwa ubabe ili kuimarisha uwekezaji na biashara nchini, lakini baadhi ya wafanyabiashara wanatumia vibaya nia hiyo njema ya Serikali kwa kukwepa kodi.


"Nilikataa kodi za dhuluma ili tuendane na misingi ya haki. Lakini inasikitisha kuona kwamba wafanyabiashara wetu sasa wamegeuza, tumekataa kodi za dhuluma kama serikali, wafanyabiashara wanafanya dhuluma ya kodi. Wanadhulumu kulipa kodi," Rais Samia alisema kwenye Baraza la Idi jana jijini Dar es Salaam.


Rais ameonya kuwa dhuluma ya kodi inayofanywa na baadhi ya wafanyabiashara nchini inarejesha nyuma maendeleo ya taifa.

"(Wafanyabiashara) wanadhulumu mapato ambayo yangetumiwa kuhudumia wananchi," amesisitiza.


"Wanafanya hivyo kwa sababu mbalimbali, labda za kisiasa, kiuchumi ili wapate utajiri zaidi, wapate mapato zaidi au uhujumu kwa makusudi kuendelea kuhujumu maendeleo ya wananchi. Niwasihi waache dhuluma hiyo inayochelewesha maendeleo ya nchi yetu na sote tuwe raia wema na tutimize wajibu wetu."


Rais Samia amesema kuwa licha ya ukwepaji kodi unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu, makusanyo ya ndani yanaendelea kuongezeka chini ya Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA).


Makusanyo ya kodi yamepanda kutoka Shilingi trilioni 18 mwaka 2020/21 wakati anaingia madarakani hadi Shilingi trilioni 24 kwa mwaka wa fedha wa 2022/23, amesema.

"Nitumie fursa hii kuwapongeza wafanyabiashara wote wanaotoa risiti wanavyouza na wananchi wote wanaoendelea kudai risiti wanaponunua bidhaa," Rais Samia amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post