AKAMATWA KWA KUISHI NA MWILI WA MAREHEMU MME WAKE AKISUBIRI AFUFUKE


Mwanamke anazuiliwa na polisi baada ya kupatikana na mwili wa marehemu mume wake uliokuwa ukiharibika katika Kaunti ya Kajiado nchini Kenya.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 58 amegunduliwa kuwa alihifadhi mwili huo katika shamba lao la Sifa viungani mwa mji wa Kitengela, runinga ya Citizen iliripoti. 

Polisi waliopokea taarifa kutoka kwa majirani wa mwanamke huyo, walivamia boma hilo na kuupata mwili huo uliokuwa ukioza. 

Malalamiko ya wenyeji wa Kitengela kuhusu uvundo 

Majirani walikuwa wamevumilia uvundo mkali kutoka kwa nyumba hiyo kwa muda kabla ya kuwasiliana na polisi.

Polisi walivamia nyumba hiyo baada ya majirani kuwafahamisha kuhusu uvundo uliotoka kwa boma la mwanamke huyo. Waliikuta maiti hiyo juu ya kitanda pale sebuleni. 

“Polisi waliingia ndani ya boma na kumkuta mwanamke huyo akiwa peke yake. Alionekana mgonjwa, amechoka na amedhoofika. 

Alikuwa akitetemeka sana,” chanzo kilifichua Citizen TV. Akihojiwa, mwanamke huyo ambaye ni Mtanzania, alifichua kuwa alikuwa akisubiri kufufuka kwa mumewe, hivyo kusita kuuzika mwili wake.

Kulingana na majirani hao, wanandoa hao wasio na watoto walikuwa wa dhehebu moja kabla ya kifo cha mwanaume huyo. 

Mwanamke huyo alipelekwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Mafunzo na Rufaa ya Mathari ili kufanyiwa uchunguzi wa kiakili huku mwili wa marehemu ukihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City kabla ya kuzikwa Nyeri. 

Kama ilivyo katika kanuni ya adhabu ya Kenya, ni kosa kwa mtu kuzuia isivyo halali kuzikwa kwa maiti.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post