BASI LAPATA AJALI LIKISAFIRISHA WANAFUNZI

Basi la Easy Coach lililokuwa likisafirisha wanafunzi kutoka Shule ya Upili ya Wavulana ya Chavakali kuelekea Nairobi limehusika katika ajali kwenye Barabara Kuu ya Kisumu-Kakamega nchini Kenya.


Ajali ya Jumatatu, Aprili 1, 2024 jioni ilitokea karibu na mzunguko wa Kanisa la Coptic karibu na Mamboleo huko Kisumu.

 Mwanafunzi katika eneo la tukio alisema walikuwa wamefunga shule na walikuwa wamepanda basi kutoka shuleni kuelekea Nairobi.

 Video kutoka eneo la tukio zinaonyesha umati wa watu wakizunguka huku wakijaribu kuwavuta wanafunzi kutoka kwa basi lililopinduka.

Wakaazi katika eneo la tukio wameelezea hofu kuwa huenda baadhi ya wanafunzi hao wamefariki lakini wanatumai matokeo mazuri zaidi huku wakiendelea na shughuli za uokoaji.

 Pia kuna hofu kuwa gari hilo huenda likashika moto huku likiendelea kuvuja mafuta wenyeji wakijaribu kuyaokoa maisha ya wanafunzi hao.


Ajali hiyo inajiri siku chache baada ya wimbi la majonzi kukumba jamii ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kufuatia ajali mbaya iliyosababisha vifo vya wanafunzi 11 na wengine kadhaa kujeruhiwa katika Barabara Kuu ya Mombasa-Nairobi. 

Kisa hicho kilitokea Jumatatu jioni, Machi 18, eneo la Maungu huko Voi wakati trela ilipogonga basi lao upande wa kushoto. 

Ajali hiyo ilipotokea, basi la shule lilikuwa limebeba wanafunzi wa afya ya umma wakielekea Mombasa kwa safari ya kimasomo.

 Wanafunzi 11 walifariki katika ajali hiyo, huku kadhaa wakijeruhiwa vibaya na kukimbizwa haraka katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Moi mjini Voi kwa matibabu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post