WAZAZI WATAKIWA KUWAELIMISHA VIJANA NAMNA YA KUJIKINGA NA MAAMBUKIZI YA VVU



Na Mwandishi wetu- SINGIDA

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amewataka wazazi kuwa karibu na vijana kuwaelimisha namna ya kujikinga na maambukizi ya VVU.

Mhe. Ummy ameyasema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mkoani Singida, walipotembelea Konga ya WAVIU ya Halmashauri ya Singida Vijijini  ikiwa ni sehemu ya kutembelea miradi inayotekelezwa na wadau kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).

Naibu waziri Ummy amesema maambukizi ya VVU yanapungua  lakini  kwa makundi ya vijana na hasa kwa wasichana bado kasi ya maambukizi inaongozeka, hivyo wazazi na walezi hawana budi kutoa elimu kwa  vijana ili kupata hamasa ya  kupima Afya zao.

“Tuwaelimishe vijana namna ya kujikinga na maambukizi ya VVU, pia wasisitizieni wakapime wafahamu afya zao iwapo watakutwa na maambukizi watashauriwa kuanza dawa mapema,”alisema Mhe. Ummy.

Aliongeza kuwa Serikali inatoa dawa bila malipo, na dawa zipo za kutosha kwa ajili ya wananchi wake juhudi ambazo zinafanywa na Seraikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassanya kuhakikisha  wananchi wanapata huduma bora ya afya.

Aidha, amewahimiza wanaume kufanya maamuzi ya kwenda kupima Afya, kwani taarifa za awali za utafiti wa viashiria vya UKIMWI ya mwaka 2022/23 zinaonesha mwamko wa wanaume kupima afya bado upo chini.

“Nawaasa akina baba nendeni mkapime afya zenu,ukikutwa na maambukizi utaanza kutumia dawa na utaishi kwa malengo,”Alieleza.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Stanslaus  Nyongo alimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha  kwa ajili ya huduma za Afya ambazo zinawezesha watanzania kuwa na Afya bora huku akimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Singida kwa kukusanya mapato ya ndani na kutenga fedha asilimia 10 kwa ajili ya kutoa mkopo wenye riba nafuu kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.

“Suala la UKIMWI ni mtambuka na ndio maana likawekwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye ndiye Mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali hivyo wizara zote ni lazima kutekeleza shughuli za UKIMWI,”Alibainisha Mwenyekiti huyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Konga ya Halmashauri ya Singida Vijijini Bw. Selemani Linja, alisema Konga ya Halmashauri ya Singida inatekeleza afua za UKIMWI kwa kushirikiana kwa karibu na uongozi wa Halmashauri na wadau mbalimbali kwa lengo la kuratibu masuala yanayohusu watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI.

“Shughuli tunazozifanya ni Kuhamasisha jamii kupima afya kwa hiari,  Kutoa elimu ya VVU na ufuasi sahihi wa dawa kwa WAVIU,  Kupinga unyanyapaa kwa WAVIU, Kuwakilisha WAVIU vijana na watu wazima katika majukwaa mbalimbali ya mwitikio wa UKIMWI ikiwa ni pamoja na Kamati za Kudhibiti UKIMWI ngazi zote pamoja  na Kuunda vikundi vya WAVIU kwa lengo la kutoa elimu rika ya matumizi ya huduma za tiba na matunzo na kuinuana kiuchumi,”Alifafanua Mwenyekiti huyo.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Jerome Kamwela alishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kwa kuendelea kufuatilia na kushauri juu ya utekelezaji wa shughuli za Mwitikio wa UKIMWI Nchini, na kuahidi kuendelea  kutekeleza ushauri na maagizo wanayonayotolewa na Kamati hiyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post