TTCL YAKABIDHI VIFAA VYA USAFI SOKO LA MABIBO

 


Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam

Wanawake wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) leo Machi 7,2024 wametoa msaada wa Vifaa vya usafi katika Soko la Mabibo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa utoaji wa vifaa hivyo ,Afisa Uhusiano kutoka TTCL Bi. Adeline Berchimance amesema lengo la kutoa vifaa katika soko la Mabibo ni kuhakikisha Wafanyabiashara wanafanya shughuli zao katika mazingira safi na salama kwa kuzingatia afya zao na wale wanaotembelea katika soko hilo kununua mahitaji mbalimbali.

“Kuelekea Kilele cha siku ya wanawake Duniani tumeona ni vyema kuendeleza utoaji wa misaada mbalimbali kama shirika na mwaka huu 2024 imeangukia hapa katika soko la mabibo wakati mwaka jana tulienda kuwaona wagonjwa pale Ocean Road na mwaka juzi 2022 tulienda shule ya Uhuru Mchanganyiko” amesema Adeline
 


Pia Bi. Adeline amesema kuwa wanawaunga mkono Wanawake wanaofanya biashara zao katika soko hilo na wengine wanaopita katika soko hilo kwa ajili ya kununua bidhaa za kwenda kutumia majumbani na vifaa hivyo vitasaidia katika usafi ili kuhakikisha wanakuwa salama.
 

Ametoa wito kwa Taasisi zingine kuona umuhimu wa kutoa msaada katika maeneo ya masoko ili kuendelea kuwaunga mkono wanawake wenzao wanaofanya biashara zao katika masoko mbalimbali na kuchangia katika kuboresha mazingira.

Naye Meneja wa soko hilo Geophrey Ngwamo amelishukuru Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa kutoa msaada huo wa vifaa hivyo ambapo vitasaidia katika utunzaji wa mazingira na kusema kuwa soko hilo la Mabibo ni kati ya masoko makubwa katika jiji la Dar es Salaam ambalo linazalisha taka nyingi. 

“Kwa vifaa hivi itatusaidia sana katika kusafisha na kutunza mazingira ikiwemo pia kuhakikisha afya ya watumiaji wa bidhaa kutoka katika soko letu zinalindwa kwa kutumia bidhaa bora na salama,” amesema Ngwamo


Kwa upande wa Wafanyabiashara wa Soko hilo wameahidi kuvitunza vifaa hivyo ikiwemo kuzingatia matumizi yake na kuvitumia kufanya usafi wa uhakika na kutunza mazingira ya soko kwa ujumla.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post