TANAPA KUANDAA ANDIKO LA KITAALAM KUWEZESHA UKARABATI MIUNDOMBINU YA SERENGETI


Baadhi ya Maofisa wa TANAPA wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi kwenye mkutano wa waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya utalii na miundombinu leo Machi 10,2024 Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi akizungumza kwenye mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya utalii na miundombinu.


Na Dotto Kwilasa,Dodoma


Serikali kupitia Shirika la hifadhi za Taifa(TANAPA)imesema inaandaa andiko la kitaalam la kuwasilisha kwenye
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuhusiana na suala la kuweka tabaka gumu kwenye miundombinu ya hifadhi ya Serengeti ambayo imo katika Orodha ya Urithi wa Dunia inayosimamiwa na Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO ili kuinusuru na uharibifu wa mazingira.


Hatua hii ni kutokana na Mvua zinazoendelea kunyesha za El Nino ambazo zimeleta athari ya uharibifu wa miundombinu ikiwemo barabara za kwenye hifadhi za taifa zilizo chini ya TANAPA


Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi ameeleza hayo Jijini hapa leo Machi 10, 2024 kwenye mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya utalii na miundombinu baada ya mvua kunyesha kwenye hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ipo chini ya Shirika la hifadhi za Taifa(TANAPA.


Amesema njia ya kutumia andiko la kitaalam ndiyo iliyotumiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) ambapo sasa imepata kibali cha kujenga barabara yenye tabaka gumu na kufafanua kuwa barabara hiyo ndiyo ndiyo inayoingia hifadhini Serengeti kwa kuzingatia kuwa vivutio hivi viwili maarufu duniani vinapakana.

"Kuna barabara kuu nne zenye changamoto zaidi kutokana na upitaji wa magari makubwa ya abiria na mizigo yanayokwenda mikoa ya jirani ya Mara, Arusha, Manyara, Mwanza, Shinyanga na Simiyu ambazo TANAPA ndizo inazozilenga katika mkakati wake wa mbinu mbadala ya tabaka gumu iwapo itakubalika, "amesema

Amesema kutokana na mvua hizo tayari TANAPA katika hatua za awali tayari imekamilisha matengenezo ya barabara na sasa barabara hizo zinapitika na watalii wanaendelea kupata huduma zinazostahili.

Amesema hakuna changamoto kubwa iliyotokea kwenye upande wa viwanja vidogo vya ndege saba vilivyopo zaidi ya maji kujaa kwenye baadhi ya maeneo ya kuegeshea ndege.


"Kwa hatua za kati TANAPA inataka kunyanyua barabara nzima ya Golini – Naabi – Seronera (km 68) kwa wastani wa sentimita 50 (nusu mita) kufuatana na ukaguzi uliyofanyika ili kuifanya iwe juu kidogo ya usawa wa ardhi, hivyo kuruhusu maji kutoka barabarani yapite kwenye mifumo ya mifereji na mitaro maji iliyopo pembezoni mwa barabara,Kazi hii inaendelea, "amesema

Msemaji huyo wa Serikali pia ameeleza kuwa kwa kuzingatia kuwa kuna visababishi na viashiria vingine vya mvua kubwa, bado mvua hizi zitakuwa ni za wastani au zaidi, ikimaanisha mvua zitakuwa kubwa kuliko ilivyozoeleka.

" Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambayo pia imeathirika na El Nino, ni hifadhi ya pili kwa ukubwa nchini yenye kilomita za mraba 14,763,hifadhi kubwa zaidi nchini ni Ruaha yenye kilomita za mraba 19,822 lakini Serengeti ndiyo hifadhi ya kwanza nchini kwa kuingiza watalii wengi zaidi,hadi sasa, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeshinda Tuzo ya Hifadhi Bora Afrika kwa miaka mitano mfululizo, "amesema.

Pamoja na mambo mengine ameeleza kufuatia kuwa hifadhi za taifa 21 zilizo chini ya TANAPA zina barabara zenye urefu wa jumla ya kilomita 16,470.6 ambapo Serengeti peke yake ina jumla ya kilomita 3,176.

"Kimsingi ndiyo hifadhi yenye mtandao mrefu zaidi wa barabara ambazo ni za udongo ama changarawe,barabara hizi zimegawanyika katika barabara kuu zilizo chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) na kundi la pili la barabara ndogondogo zilizo chini ya TANAPA yenyewe, "amefafanua

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post