SERIKALI YAELEZA NAMNA KASI YA UTATUZI WA CHANGAMOTO ZA MUUNGANO ILIVYOONGEZEKA

 

Na Dotto Kwilasa, DODOMA

WAZIRI wa Nchi OFisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Selemani Jafo amesema kuwa kasi ya utatuzi wa changamoto imeongezeka ambapo hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 25 zilizoibuliwa ambapo ni sawa na asilimia 60.

Waziri Jafo ameeleza hayo leo March 26,2024 jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo alisema serikali zetu mbili zimeweka mwongozo rasmi wa vikao vya kamati ya pamoja ya kushughulikia masuala ya Muungano ambavyo hushirikisha wajumbe kutoka pande zote mbili za Muungano.
 
"Tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa vikao vya pamoja mwaka 2006 hadi sasa, kasi ya utatuzi wa changamoto imeongezeka ambapo hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 25 zilizoibuliwa,changamoto nyingi ambazo zilikuwa hazijapatiwa ufumbuzi zimejadiliwa na pande zote mbili za Muungano na kupatiwa ufumbuzi ambapo katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024 pekee hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 18 zilizokuwepo kwa kipindi hicho, "amesema. 

Pamoja na hayo alisema hoja zilizobakia nne zipo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi.

"Hoja hizo Mbili zinahusu sekta ya fedha ,ambao mgao wa mapato kutoka hisa bodi ya sarafu ya Afrika Mashariki na mgawanyo wa faida kutoka benki kuu .

Kero nyingine ni kero ya usafiri wa vyombo vya moto, kwamba mtu akija na gari yake Tanzania Bara aweze kutembea muda wote na uletaji wa sukari kutoka kiwanda cha mahonda Zanzibar katika soko la Tanzania bara.

Katika hatua nyingine Waziri Jafo alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeendelea kushirikiana katika kuibua na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

 Miradi hiyo imechangia kupunguza umaskini wa kipato na kuinua ubora wa maisha na ustawi wa jamii wa pande zote mbili za Muungano. 

"Miongoni mwa miradi na programu zilizotekelezwa na kukamilika pande mbili za Muungano ni pamoja na miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF awamu ya I hadi III, Programu ya Usimamizi wa Bahari na Pwani (MACEMP), Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP), Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo na Sekta ya Mifugo (ASDP – L), Programu ya Kuwezesha Sekta ya Kilimo (ASSP), na Programu ya Changamoto za Milenia (MCA – T).
 
Miradi mingine ni Mradi Shirikishi wa Programu za Maendeleo ya Kilimo (PADEP); Mradi wa Udhibiti wa Uvuvi na Maendeleo Shirikishi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH), Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani ya Mazao na uboreshaji wa huduma za Fedha Vijijini (MIVARF), 

Mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji wa Zao la Mpunga (ERPP); Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika Maeneo ya Pwani (LDCF); na Mradi wa Kurejesha Ardhi Iliyoharibika na Kuongeza Uhakika na Usalama wa Chakula katika Maeneo Kame ya Tanzania.
 
Programu na miradi inayoendelea kutekelezwa pande mbili za Muungano ni pamoja na miradi ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo (CDCF), Mradi wa Ujenzi wa Kingo za Kuzuia Maji ya Bahari na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia ya Vijijini (EBARR).

Pamoja na hayo alitaja mafanikio ya miaka 60ya Muungano kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa shule za msingi kutoka shule 3,270 mwaka 1961 hadi shule 20,562 mwaka 2024, ambapo kati ya hizo, shule za Serikali ni 18,012 na za binafsi ni shule 2,550.

Shule za Sekondari nazo zimeongezeka kutoka shule 41 mwaka 1961 hadi shule 6,511 mwaka 2024, kati ya hizo, shule 4,892 ni za serikali na 1,619 ni za binafsi. 

Lakini pia Vituo vya kutolea huduma za afya ngazi zote vimeongezeka kutoka vituo 1,343 mwaka 1960 hadi vituo 9,662 mwaka 2024.

 Kati ya vituo hivyo, Zahanati ni 8,043; Vituo vya Afya 1,176; Hospitali za Halmashauri 171; Hospitali zenye hadhi ya Wilaya 182; Hospitali za Rufaa za Mikoa 28; Hospitali zenye hadhi ya Mkoa 34; Hospitali za Rufaa za Kanda 5; Hospitali zenye hadhi ya Kanda 11; Hospitali maalumu 6; Hospitali ya Taifa 1; na Hospitali Maalumu za Taifa 6. 

Alosema upatikanaji wa maji vijijini umeongezeka kutoka asilimia 32 mwaka 2000 hadi asilimia 77 mwaka 2022. Aidha, upatikanaji wa umeme umeongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2000 hadi 78 mwaka 2022. 

Vile vile, mtandao wa barabara za lami na zege mijini na vijijini umeongezeka kutoka KM 1,360 mwaka 1961 hadi KM 11,966 mwaka 2022.  

Utoshelezi wa chakula umeongezeka kutoka asilimia 90 mwaka 2000 hadi asilimia 124 mwaka 2022. Vile vile, udugu na uhusiano wa wananchi umeendelea kuimarika ambapo wananchi wa pande zote mbili wameungana katika misingi ya ndoa na kujenga urafiki katika uendeshaji wa shughuli za kibiashara na kijamii.

Aidha alisema kuwa mwenendo wa ukuaji wa uchumi katika kipindi cha miaka 60 umekuwa ni wa kuridhisha ambapo Pato Ghafi la Taifa limeendelea kukua na kufikia shilingi trilioni 170.3 mwaka 2022 kutoka shilingi trilioni 156.4 mwaka 2021. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post