SEKRETARIETI YA MAADILI NENDENI MKASIKILIZE MALALAMIKO YA WANANCHI-WAZIRI SIMBACHAWENE

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiongea na maafisa uchunguzi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika kikao kazi cha wachunguzi Kilichofanyika katika ukumbi wa Ngorongoro jijini Arusha tarehe 18 Machi 2024.

Kamishna wa Maadili, Jaji (Mst.) Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi akiongea na maafisa uchunguzi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika kikao kazi cha wachunguzi Kilichofanyika katika ukumbi wa Ngorongoro jijini Arusha tarehe 18 Machi 2024.

..........

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (Mb) ametoa wito kwa watumishi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Umma kutoka ofisini kwenda kwa wananchi kusikiliza malalamiko yao na kuyatafutia ufumbuzi badala ya kukaa ofisini kusubiri wananchi wachache wanaolalamikia viongozi.

“Sekretarieti ya Maadili nendeni mkawasilikize wananchi, yapo mambo wanayapigia kelele sana kuhusu tabia na mwenendo wa viongozi wao. Kelele zao zinaposikika tokeni mkawasikilize, hii itasaidia kutatua kero zao na mtawasaidia pia viongozi kujirudi na kufuata misingi ya maadii,” alisema.

”Tusichelewe sana kushughulikia malalamiko yanayotolewa na wananchi hadhalani.”

Mhe. Simbachawene alisema hayo jijini Arusha tarehe 18 Machi, 2024 wakatiakifungua kikao kazi cha Wachunguzi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadii ya Viongozi wa Umma.

“Misingi hii lazima tuilinde na hili ndilo jukumu letu. Misingi hii isipozingatiwa, wananchi wanakosa huduma na malengo ya nchi hayatafikiwa,” alisema.

Kwa mujibu wa Mhe. Waziri, lazima watumishi wa Sekretarieti ya Maadili watoe elimu kuhusu misingi ya maadli na kusikiliza changamoto zao.

Katika hatua nyingine Mhe. Simbachawene alisema jukumu la kusimamia maadili linahitaji mtumishi anayetumia mbinu, busara na weledi wa hali ya juu kutokana na kuwahusu viongozi wakubwa na ni la kikatiba.

“Maadili ni zaidi ya sheria, lazima msimamie maadili ya viongozi wote kuanzia ngazi ya chini. Twende mbali tuanzie ngazi ya chini huko serikali za mitaa kusimamia maadili. Tusihangaike na viongozi wanaojaza fomu za Tamko tu kwasababu lazima kiongozi yeyote lazima awe mwadilifu,” alisema na kuongeza kuwa, “maadili katika jamii zetu ni jambo la msingi na lilikuwepo hata wakati wa ujima.”

Awali akimkaribisha Mhe. Waziri, Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Sivangilwa Mwangesi alieleza kuwa Taasisi imeona umuhimu wa wachunguzi wote kuwa na kikao cha pamoja kujadili mustakabali wa majukumu yao.

“Hii ni mara yetu ya kwanza tangu Taasisi ilipoanzishwa mwaka 1996 kuwa na kikao kama hiki kwa lengo la kuwakutanisha wachunguzi wote ndani ya Taasisi kujadili kwa kina mambo mbalimbali yanayohusu utendaji wa kazi na mafanikio kwa mujibu wa matakwa ya Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,” alisema.

Kwa mujibu wa kifungu cha 19(2) cha Sheria ya Maadili ya Viongizo wa Umma Na. 13 ya 1995, majukumu ya Sekretarieti ya Maadili ni kupokea malalamiko ya ukiukwaji wa maadili, kufanya uchunguzi, kupokea matamko, kufanya uhakiki na kutoa elimu ya maadili.

Majukumu mengine ni kufanya utafiti wa hali ya uadilifu nchini, kutoa ushauri katika mambo ya uadilifu na kubuni mikakti ya ukuzaji maadili.

Mhe. Sivangilwa alizitaja mada zitakazo wasilishwa kuwa ni; Utendaji katika Ofisi za Kanda, Viambata vya Makosa ya Maadili, Utaratibu wa zoezi la Uhakiki, Mikakati ya utendaji kazi pamoja na Changamoto na utatuzi wake katika kushughulikia malalamiko na uchunguzi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post