Mkurugenzi Mtendaji anayemaliza muda wake wa Foundation For Civil Society (FCS), Francis Kiwanga akizungumza katika mkutano maalum wa wadau wa AZAKI kwaajili ya kutoa maoni yao kwenye rasimu ya Dira ya Taifa ya maendeleo 2050 Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa kikosi kazi cha ukusanyaji maoni cha AZAKi chini ya uratibu wa Foundation for Civil Society (FCS), Wakili Imelda Lulu Urio, akiwasilisha mapendekezo ya AZAKI katika mkutano huo
DAR ES SALAAMAsasi za Kiraia nchini (AZAKi) zimewasilisha mapendekezo tisa ya rasimu yao ya awali kwa ajili ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa Kamati ya Taifa ya Uandaaji wa dira hiyo.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika leo Machi 15, 2024 Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa kikosi kazi cha ukusanyaji maoni cha AZAKi chini ya uratibu wa Foundation for Civil Society (FCS), Wakili Imelda Lulu Urio ametaja matarajio makuu tisa yaliyopendekezwa kwenye rasimu hiyo, la kwanza likiwa ni maisha bora na ustawi wa Watanzania.
Tarajio la pili amesema ni mazingira ya haki, amani, usalama na umoja; Tatu Utawala bora na Uwajibikaji; Nne, jamii iliyoelimika na shindani kwa viwango vya kikanda na kimataifa; na tano akasema ni uchumi anuai na jumuishi unaozingatia ukuaji wa uchumi na ustahimilivu, kuimarisha usawa wa kijamii (social equity), usawa wa kijinsia kiuchumi, kisiasa na kuongeza ajira kupitia sekta za kipaumbele. Tarajio la sita ametaja kuwa na Taifa lenye fahari linalojivunia uadilifu, mila na desturi chanya kwa ujenzi wa Taifa la kisasa linalozingatia Utanzania na Uafrika. Saba akasema ni ulinzi, usimamizi na uendelezaji wa rasilimali, kipaumbele kikiwa ni matumizi na usimamizi endelevu wa rasilimali za nchi. Tarajio la nane amesema ni kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa maendeleo endelevu na tarajio la tisa ni kuwa na jamii yenye uwezo wa kutumia na kunufaika na teknolojia.
Mapendekezo hayo yametokana na asasi mbalimbali kutoka Tanzania bara na visiwani ambapo zaidi ya asasi 120 zimetoa maoni kwa njia ya mtandao (digital survey tool), asasi 40 zimeshiriki maoni kupitia majadiliano ya vikundi (Focus Group Discussions - FGD) na asasi 100 zimeshiriki kwa njia ya warsha.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya uandaaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, amewashukuru wana AZAKi kwa maoni yao mazuri na kwamba yatasaidia kupatikana kwa Dira bora ya 2050 itakayokidhi mahitaji ya kila sekta na kukuza ufanisi wa maendeleo endelevu na jumuishi kwa kila Mtanzania na kuondoa changamoto ambazo hazikutekelezwa na dira ya 2025 inayokamilika juni mwakani.
Aidha, Balozi DKt. Migiro, ametoa rai kwa wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kutoa mapendekezo zaidi kwani muda bado ni mwingi kwa wadau kuchangia.
Zoezi la kukusanya maoni jumuishi la Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 lilifunguliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan Desemba 9, 2023.