RC MNDEME AONGOZA KIKAO CHA KAMATI YA USHAURI YA MKOA WA SHINYANGA, ATAHADHARISHA KIPINDUPINDU, BEI YA SUKARI


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akiongoza kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Shinyanga (RCC leo Alhamisi Machi 7,2024 katika ukumbi wa Chuo cha Walimu Shinyanga (Shycom).  Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akizungumza wakati akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Shinyanga (RCC) leo Alhamisi Machi 7,2024 katika ukumbi wa Chuo cha Walimu Shinyanga (Shycom). 

 Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amewaagiza Maafisa Afya mkoani Shinyanga kuhakikisha sehemu zote zenye mikusanyiko ya watu kuwe na maji tiririka ya kunawa mikono na kuchukua hatua za kisheria pale watakapojiridhisha kuna mtu kwa maksudi hataki kufuata kanuni za afya na hivyo kusababisha ugonjwa wa kipindupindu kuendelea kusambaa.

Mhe. Mndeme ametoa agizo hilo leo Alhamisi Machi 7,2024 wakati akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Shinyanga (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Walimu Shinyanga (Shycom) kikilenga kujadili mambo mbalimbali kuhusu Mkoa wa Shinyanga. 

Mhe. Mndeme ugonjwa wa kipindupindu bado upo ndani ya Mkoa wa Shinyanga katika baadhi ya halmashauri ambapo mpaka sasa kati ya wagonjwa 216 walioripotiwa, wagonjwa 127 wamekutwa na vimelea vya kipindupindu hivyo kuagiza hatua madhubuti zichukuliwe ili kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa wa kipindupindu.

"Halmashauri mbili zimeweza kuudhibiti ugonjwa wa kipindupindu ambazo ni Manispaa ya Kahama (siku 29 hawana mgonjwa) na Halmashauri ya Kishapu (siku 9 hawana mgonjwa). Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imeendelea kupata wagonjwa kipindupindu baada ya kukaa kwa muda wa siku 13 bila wagonjwa (Februari 12- 25,2024.  Na kwa Manispaa ya Shinyanga kata za Ndala na Kambarage zimeathirika zaidi",amesema Mhe. Mndeme.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema pia bado mkoa wa Shinyanga unakabiliwa na changamoto ya kupanda kwa bei ya sukari hivyo amewaelekeza Mawakala wote wanaouza sukari ndani ya mkoa wa Shinyanga waendelee kuzingatia maelekezo ya serikali kwa kuuza sukari kwa bei elekezi ambapo bei ya rejareja ni kati ya shilingi 2,800/= hadi 3,000/= kwa kilo moja na kwa bei ya jumla ni kati ya shilingi 2,650/= hadi 2,800/= ambapo kwa mfuko wa kilo 50 ni kati ya shilingi 132,500/= na shilingi 140,000/=.

Mhe. Mndeme pia ameziagiza Halmashauri kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wafugaji ambayo hayataathiri shughuli za kilimo na mazingira ili kuongeza uzalishaji wa ng'ombe, mbuzi na kondoo kutokana na kwamba Shinyanga kuna Machinjio ya kisasa huku akiwataka  maafisa mifugo kutembelea wafugaji na kuwapa elimu ya ufugaji wa kisasa hali ambayo italeta mazingira rafiki kwa wafugaji waache kuhama mkoa kwenda kutafuta malisho.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile.

Akitoa taarifa ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwa Mkoa wa Shinyanga, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu ikiwemo kuepuka kula chakula kwenye misongamano ikiwemo kwenye misiba huku akieleza kuwa hivi sasa Manispaa ya Shinyanga ndiyo ina wagonjwa wengi wa kipindupindu ambapo Mto wa Ndala umebainika kuwa na vimelea vya ugonjwa huo.

Dkt. Ndungile amesema Halmashauri za Manispaa ya Kahama, Kishapu hali imeanza kutengamaa isipokuwa Manispaa ya Shinyanga ambayo bado ina wagonjwa na maeneo yaliyoathirika ni kata ya Ndala na Kambarage.

"Jumla ya visa vilivyoripotiwa katika Manispaa ya Shinyanga ni 43 , wagonjwa waliopo kitandani ni watano, walioruhusiwa ni 38. Jumla ya watu walitengamana na wagonjwa ni 109",amesema.

Naye Mbunge wa Kishapu Mhe. Boniphace Butondo amefikisha kilio cha wakazi wa Kishapu kuhusu ujenzi wa barabara ya Kolandoto Mhunze kwani imekuwepo kwenye Ilani ya CCM lakini utekelezaji wake umekuwa ukisuasua ambapo katika kikao cha RCC kiliazimia kuunda timu  kufuatilia ngazi za juu kuhusu ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami lakini bado utekelezaji wake haujafanyika.

Katika kikao hicho cha RCC, mbali na wajumbe kujadili masuala mbalimbali kuhusu maendeleo ya mkoa, pia taarifa mbalimbali zimewasilishwa ikiwemo taarifa ta Mpango na Bajeti ya Mkoa wa Shinyanga kwa mwaka wa fedha 2024/2025, taarifa ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwa Mkoa wa Shinyanga, taarifa ya sukari, taarifa ya sekta ya maji RUWASA, KASHWASA, KUWASA na SHUWASA, taarifa ya usambazaji wa huduma za umeme na taarifa ya sekta ya miundombinu (TANROADS na TARURA).

Kikao hicho  pia kimeazimia kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya kuwaletea maendeleo wananchi wa mkoa wa Shinyanga na Tanzania kwa ujumla ambapo vijiji vyote 506 katika mkoa wa Shinyanga vimefikiwa kwa miradi ya maendeleo. 

Hali kadhalika kikao hicho kimezielekeza halmashauri za wilaya katika mkoa kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuwaagiza watalaamu wa kilimo katika halmashauri kuja na mkakati wa kuwezesha wafugaji kuwa na malisho bora pamoja na namna ya kutibu mifugo yao ili iwe na tija.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akizungumza wakati akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Shinyanga (RCC) leo Alhamisi Machi 7,2024 katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Shinyanga (Shycom). Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akizungumza wakati akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Shinyanga (RCC) leo Alhamisi Machi 7,2024 katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Shinyanga (Shycom).
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akizungumza wakati akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Shinyanga (RCC) leo Alhamisi Machi 7,2024 katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Shinyanga (Shycom).
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akiongoza kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Shinyanga (RCC) 
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akiongoza kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Shinyanga (RCC
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Prof. Siza Tumbo akizungumza wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Shinyanga (RCC) leo Alhamisi Machi 7,2024 katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Shinyanga (Shycom).






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments