GGML YAWAPA MBINU WANAFUNZI GEITA BOYS KUFIKIA MALENGO YA KITAALUMA


Scholastica Kabonge -Ofisa wa masuala ya ulinzi shirikishi na usalama kutoka GGML (katikati), akiwapatia ushauri na uzoefu wake wa kitaaluma wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Geita kama sehemu ya Mpango wa GGML Mentorship Programme.
Andrew Mazula, Ofisa Utumishi kutoka Idara ya Rasilimali Watu - GGML, akizungumza na wanafunzi wa sekondari ya wavulana Geita kuhusu masuala muhimu wanayotakiwa kuzingatia ili kufikia mafanikio na malengo yao kitaaluma.
Na Mwandishi Wetu

Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetoa mafunzo maalumu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Geita (Geita Boys) kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi hao kutambua masomo sahihi wanayoyamudu na fani zinazoendana na masomo hayo katika soko la ajira.

Mafunzo hayo yametolewa wiki iliyopita mkoani Geita na baadhi ya wafanyakazi wa GGML wakiwamo wanawake wanaounda kundi la GGM Ladies ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya sherehe za siku ya wanawake duniani.


GGML ladies imetoa mafunzo hayo ya siku moja kupitia program maalumu ya ushauri na usimamizi iliyopewa jina la (GGM Mentorship Program) kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi hao wa kidato cha kwanza hadi cha tano, kutambua uwezo wao kielimu na malengo waliyojiwekea katika kutimiza ndoto zao.

Akizungumza na wanafunzi hao, Ofisa wa masuala ya usafirishaji kutoka idara ya Rasilimali watu, Laila Mohamed alisema huu sio muda wa wanafunzi kufuata mkumbo katika kuchagua masomo ya kusoma na kufikia malengo yao kimaisha.

“Ili kufikia malengo ya kitaaluma, hiki sio kipindi cha kufuata mkumbo... kwamba ukisikia Juma amechukua biology na wewe unachukua mchepuo wa sayansi. Hiki ni kipindi cha kujitathmini na kujitafakari kwamba ni kitu gani unakimudu ili uchukue masomo sahihi kufikia lengo lako,” alisema.

Alisema wanafunzi wengi wamekuwa na changamoto ya kutokuwa na msimamizi au mshauri anayeweza kuwashauri namna ya kujinasua katika changamoto mbalimbali kitaaluma jambo ambalo GGML imeona ni vema kujaza nafasi hiyo.

Naye Joscar Rumanyika ambaye ni mhasibu kutoka GGML, aliwaonya wanafunzi hao kujiepusha na vitendo viovu vya uvunjifu wa maadili ili kutimiza malengo yao kitaalumu.

Joscar aliwataka wanafunzi hao kuwa na uthubutu na kujiamini kwamba hakuna kinachoshindikana ili kufaulu vema katika masomo yao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wanafunzi hao kutoka Geita Boys, Leonard Martin na Daniel Stanslaus walisema mafunzo waliyopatiwa na GGML yamewasaidia kutambua namna ya kufikia malengo yao.

Martin (14) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili na mkazi wa Bwanga mkoani Geita, alisema alisema elimu hiyo inawawezesha kujiandalia maisha mazuri ya baadae.

Makamu Rais Mwandamizi wa AngloGold Ashanti-GGML - Kitengo cha Ubisa/ Ushirika Afrika, Terry Stron alisema program hiyo ya mentorship inalandana na malengo ya kampuni hiyo ya kuwekeza kwa vizazi vijavyo kwani kuwekeza kwa wanafunzi hao ni sawa na kuwekeza kwa jamii ya Geita ijayo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post