SERIKALI YASAINI MKATABA WA UPEMBUZI YAKINIFU WA UNUNUZI WA MELI ZA UVUVI NA UJENZI WA VIWANDA VYA SAMAKI

 


Na Dotto Kwilasa, DODOMA

SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu)imesaini Mkataba wa upembuzi yakinifu wa ununuzi wa meli za uvuvi wa bahari kuu na ujenzi wa viwanda viwili vya kuchakata samaki Kilwa na Fungurefu utakaogharimu jumla ya Dola za kimarekani milioni 77.4

Hayo yameelezwa leo Februari 27,2024 Jijini hapa na Mratibu wa Programu ya kuendeleza kilimo na uvuvi  nchini Salimu Mwinjaka kwenye hafla ya utiaji saini Mkataba huo na kueleza kuwa mradi huo  utachukua muda wa miaka sita hadi kukamilika kwake kuanzia mwaka 2021/2022 hadi 2027/2028 . 

Amesema kati ya fedha hizo, mkopo toka IFAD ni Dola za Marekani milioni 58.8,fedha za Serikali ni Dola za Marekani 7.8,Sekta binafsi Dola za Marekani milioni 8.5 na fedha za wananchi Dola za Marekani milioni 2.4.

"Lengo kuu la Programu hii ni kuwa na uzalishaji endelevu wa kibiashara na wenye kuzingatia mazingira hususani uzalishaji wa mbegu za mazao ya kilimo ikiwemo mahindi, alizeti, maharage na mimea jamii ya kunde, uvuvi na ufugaji wa viumbe maji ukizingatia uwezeshaji wanawake na ushiriki wa vijana,"amesema

Amefafanua kuwa programu hiyo inatarajiwa kunufaisha watu takribani 1,3000,000 ikiwemo Kaya za wakulima wadogo 200,000 ambao watakuwa wanapata mbegu bora za mahindi,alizeti na maharage. 

Aidha wazalishaji wadogo na kati wa mbegu na Wafanyabiasha wa pembejeo za kilimo takribani 1,000  watapata mbegu bora na mafunzo , wavuvi wadogo na Wafanyabiasha wa samaki takribani 48,000 na wafugaji wa samaki na viumbe maji na mwani 21,000.

Pamoja na mambo mengine ameeleza kuwa Programu hiyo inaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na kutekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar kupitia Taasisi ambazo ziko chini ya Wizara hizo ikiwa ni pamoja na TAFICO , ZAFICO, Wakala wa mbegu-ASA, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo-TARI na Taasisi ya udhibiti wa ubora wa mbegu-TOSCI. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Dot. Jim Yonazi ameleeza kuwa programu ya kuendeleza kilimo na Uvuvi ni mpango wa utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi ambapo Serikali inakusudia kununua meli nane kwa ajili ya Uvuvi wa bahari kuu kwa kujumuisha meli nne kwa ajili ya TAFICO na nyingine nne kwa ajili ya ZAFICO. 

"Upembuzi yakinifu wa awali tayari umekamilika na kubainisha kuwa meli hizo za Uvuvi zitaleta tija kwenye Uchumi, kuleta mchango kwenye sekta ya Uvuvi katika pato la taifa ikiwa ni pamoja na kuboresha lishe na kipato kwa mwananchi mmoja mmoja, " amesisitiza

Dkt.Yonazi amesema,"Programu ya kuendeleza kilimo na Uvuvi ni ya kimkakati hivyo Sisi kama Serikali tutahakikisha tunasimamia kwa ukaribu zoezi zima ili kuleta ufanisi unaotakiwa ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zozote zitakazo jitokeza ili kuleta tija,hivyo, mkifanya kazi hii kwa weledi na kukamilisha kwa wakati uliopangwa mtakuwa mmeshiriki katika kutafsiri maono ya Viongozi wetu wakuu, "amesema. 

Pamoja na hayo ametumia nafasi hiyo kuzipongeza kampuni za DMG na TANSHEQ ambazo ziliingia ubia na kushinda zabuni hiyo   
na kwamba Mkataba huu  utatekelezwa kwa muda za siku zisizozidi 45 kwa gharama ya Shilingi milioni 348, huku akiweka mategemeo zaidi ya  kazi hiyo kufanyika kwa weledi na kumaliza kwa wakati. 

"Ninawasihi wakati wa utekelezaji wa zoezi hili la Upembuzi Yakinifu, mara mtakapopata changamoto yoyote, tafadhali msisite kuwasiliana na ofisi yangu kwa utatuzi wa haraka ili tuweze kukamilisha zoezi ndani ya muda tuliokubaliana,kukamilika kwa upembumbuzi yakinifu kwa wakati kutawezesha Serikali kuanza taratibu za ujenzi wa meli za uvuvi katika bahari kuu pamoja na viwanda vya kuchakata samaki,"amesema


Matukio katika picha

Hafla ya Utiaji Saini Mikataba ya Kufanya Upembuzi Yakinifu wa Kujenga Meli za Uvuvi wa Bahari Kuu  na Viwanda vya Kuchakata Samaki vitakavyojengwa Kilwa na Fungurefu iliyofanyika tarehe 27 Februari, 2024 katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dodoma.









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post