KADA YA UUGUZI NA UKUNGA YAIOMBA SERIKALI KUHARAKISHA MAPITIO YA MAPENDEKEZO YAKE

 


Na Dotto Kwilasa,DODOMA

Kada ya Uuguzi na Ukunga nchini imeiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya kuharakisha mapitio ya mapendekezo yake juu ya maboresho pendekezwa ya mgawanyo wa madaraka sawa kwenye ngazi zote kwa kuzingatia vigezo vya elimu na weledi. 

Hayo yamejiri Jijini hapa kwenye Jukwaa la mwaka linalowakutanisha wauguzi na wakunga 
Machi 18, 2024 kwa lengo la kufanya tathimini ya utekelezaji wa utendaji kazi wa utoaji wa huduma za uuguzi na Ukunga ambapo zoezi hilo lililoenda sambamba na uzinduzi wa jarida la idara ya Uuguzi na Ukunga jijini Dodoma.

Akiwasilisha mapendekezo hayo kwa Naibu Waziri wa Afya Dk. Godwin Mollel,Katibu wa Kada hiyo Moses Tawete amesema ikiwa mapendokezo hayo yatafanyiwa kazi itasaidia kuondoa mtizamo uliopo sasa wa taaluma moja kuhodhi nafasi zote katika sekta ya Afya. 

Tawete ameshauri pia zoezi la uongezaji wa vituo vya Afya uendane na ajira mpya ili kukidhi utoaji huduma kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuwekeza zaidi kwenye vifaa tiba. 

Suala la maboresho ya mfuko wa Taifa wa bima ya Afya(NHIF)halikuachwa nyuma ambapo amependekeza kuwa kitika cha mafao kijumuishe huduma za Ukunga na Uuguzi kwa manufaa ya wananchi wa hali ya chini. 

Kutokana na hayo,Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema Serikali itaangalia namna bora ya kuboresha mapendekezo hayo huku akieleza kuwa Kada hiyo ni muhimu kwa jamii na hivyo inatakiwa kuwezeshwa ili ifanye kazi kwenye mazingira mazuri.

Amesema asilimia 60 ya watumishi katika sekta ya afya nchini wanatoka  kada za uuguzi na ukunga hivyo kuchangia ubora wa huduma zinazotolewa katika Hospitali na Vituo vya kutolea huduma za afya.

Dkt. Mollel amesema kada ya Uuguzi imekuwa muhimu katika kutoa huduma bora kwa sababu asilimia 80 ya kazi za afya zinatekelezwa na kada hiyo na kutoa rai kada hiyo kujumuishwa kwenye mfumo wa utoaji wa maamuzi.

Ameongeza kuwa,"Ukiona kituo cha afya kinatoa huduna bora ni kwa sababu ya uwepo wa wauguzi ambao ndio wamekuwa watendaji wakuu ambao wanakaa muda mwingi na wagonjwa hivyo ni muhimu wakawekwa kwenye mfumo wa uongozi na utoaji wa maamuzi na uundwaji wa sera”amesema

Dkt. Mollel Ameongeza kuwa wauguzi na wakunga wanapopata fursa ya kuingia ndani ya mfumo wa uongozi watasaidia kuhakikisha mambo yanaboreshwa kwenye sekta ya Afya lakini pia maslahi yao

Kwa upande wake  Mkurugenzi wa idara ya Huduma za Uuguzi na Ukunga Bi. Ziada Sella ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuajiri Wauguzi na Wakunga zaidi ya 40,000 kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 na kuongeza kuwa  kada hiyo ina dhamana kubwa katika utoaji wa huduma hivyo wazingatie miongozo, kanuni na sheria zilizowekwa kwa maslahi ya taifa.

“Tunamshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha kuajiri wauguzi na wakunga zaidi ya elfu arobaini hii inaonyesha umuhimu na dhamana ya kada hii kwa sababu hawa ndio hutumia muda mwingi kukaa na wagonjwa.

Kikao hicho kilichowakutanisha Viongozi wauguzi na Ukunga kote nchini kimebeba kauli Mbiu isemayo “Huduma Staha na Mawasiliano ni Wajibu wa Kila Mtoa Huduma za Afya”.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Manesi Alexander Balunya amesema pamoja na kubeba jukumu zito kwenye jamii Kada hiyo bado haipewi kipaumbele na kuiomba Serikali kuhakikisha inatatua kero zote na kuweka uwekezaji unaohitajika. 

Balunya amesema , "Huduma za Uuguzi ni mtambuka hivyo wanahitaji usimamizi wezeshi, muundo wa utawala unapaswa kufanyiwa mapitio ili kuwa na muundo unaiwatambua hata pale wanapotoka kujiendeleza, hili likifanikiwa litaongeza chachu ya utoaji huduma za Ukunga na Uuguzi kwa jamii, " amesema








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post