BENKI YA CRDB YAZINDUA HUDUMA YA BIMA YENYE MISINGI YA SHARIA KWA WATANZANIA WOTE


Dar es Salaam. Tarehe 28 Februari 2024: Ikiwa na uzoefu wa takriban miaka minne sasa Benki ya CRDB imezindua huduma za bima zinazozingatia misingi ya shariah zijulikanazo kama Takaful kwa ajili ya wateja wanaofuata imani ya Kiislamu na wananchi wengine wanaozingatia misingi ya dini hiyo.

Akizindua huduma hizo, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeir ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuonyesha njia katika huduma zake kwa kutambua kwamba wapo baadhi ya wateja ambao hushindwa kupata huduma kutokana na imani zao za kidini.
“Hongereni sana kwa ubunifu huu. Shariah ni sehemu muhimu kwa waumini wa Kiislamu ingawa wapo watu wa imani nyingine wanaozipenda na kuzitekeleza kanuni na misingi ya shariah. Kwa bima hizi za Takaful, naamini mtakuwa mmekata kiu ya wengi nami nawaomba Waislamu wenzangu na watu wote wanaoifuata misingi ya shariah kulinda mali na maisha yao kwa bima za Takaful,” amesema Sheikh Zubeir.


Kwa upande wake, Kamshna wa Bima na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware amesema ubunifu unaotatua changamoto zinazowakwamisha Watanzania kutumia huduma za bima unahitajika ili kuikuza sekta hiyo na kuwawezesha wananchi wengi kuwa na uhakika wa mipango na miradi wanayoitekeleza.
“Takaful ni huduma inayowakaribisha watu wenye imani ya Kiislamu ambao hawaridhishwi na huduma za bima ya kawaida ambazo zina riba. Takaful sio tu ni huduma za bima bali uwekezaji unaomnufaisha mteja pamoja na kampuni inayotoa huduma hizo. Kwa kutumia mtandao wenu mpana wa matawi, naamini Benki ya CRDB mtazifikisha huduma hizi kila kona ya nchi,” amesema Dkt. Saqware.


Mwaka 2021 Benki ya CRDB ilianzisha kitengo maalum cha huduma zinazofuata misingi ya Shariah yaani CRDB Al Barakah Banking hali iliyoifanya kuwa benki ya kwanza nchini kufikisha huduma zinazozingatia shariah nchi nzima. Katika kipindi hicho chote mpaka sasa, CRDB Al Barakah inao wateja zaidi ya 135,000 na kufanya uwezeshaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 125, sehemu kubwa ikielekezwa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.
Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema siku zote benki inaendelea kuboresha huduma na bidhaa zake na mwaka jana ilianzisha huduma maalum ya uwezeshaji wa safari za Ibada ya Hijja na Umrah.


“Katika mwendelezo wa kuboresha huduma zetu, Benki ya CRDB kwa kushirikiana na wenzetu, Zanzibar Insurance Corporation (ZIC) Takaful, leo tunazindua huduma za bima zinazofuata misingi ya shariah maarufu kama Takaful. Hii inapelekea kwa mara nyingine CRDB kuwa Benki ya kwanza nchini kuleta huduma hizi kwa wateja wake nchi nzima,” amesema Raballa.
Akieleza tofauti ya Takaful na bima za kawaida, Raballa amesema Takaful haina malipo ya riba, imeundwa katika misingi ya kusaidiana (taawun) pale baadhi ya wahusika wanapokumbwa na majanga na inahusisha uwekezaji wa sehemu ya michango ya wateja na faida inayopatikana hugawanywa kwa wateja kwa kuzingatia taratibu zilivyoainishwa na kampuni husika ya Takaful.


“Kupitia ushirikiano huu tunakwenda kutoa huduma za bima za jumla (general insurance) ikiwamo bima za magari, bima ya nyumba, moto, biashara, bima ya usafirishaji, na bima ya mitambo. Nichukue fursa hii kuwakaribisha Watanzania wote kuchangamkia fursa hii ya bima inayofuata misingi ya shariah (Takaful) inayoenda kutolewa rasmi kupitia Benki yetu pendwa ya CRDB. Takaful ni kwa ajili ya mtu yoyoye anayetamani kupata bima inayofuata misingi ya Shariah na inapatikana katika matawi yetu yote yaliyosambaa nchi nzima,” amesema Raballa.
Afisa Mtendaji Mkuu wa ZIC Takaful, Said Abdallah Basleym amesema ni furaha kwao kushirikiana na Benki ya CRDB, taasisi kubwa nchini kusambaza huduma za Takaful kwa Watanzania.


“Mshikamano huu naamini utasaidia kuzifikisha kwa wananchi wengi zaidi huduma za Takaful. Tutaendelea kushirikiana na wadau wengine wenye nia ya dhati ya kueneza huduma hizi kwa manufaa ya kila Mtanzania. Bima ndio namna pekee ya kulinda mali, biashara au afya ya mtu hivyo kila mmoja wetu anastahili kuwa nayo bila kikwazo cha aina yoyote,” amesema Basleym.


Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Al Barakah, Abdul Mohamed (kushoto) akizungumza wakati wa hafla yaa uzinduzi wa huduma za bima zinazozingatia misingi ya shariah zijulikanazo kama Takaful kwa ajili ya wateja wanaofuata imani ya Kiislamu na wananchi wengine wanaozingatia misingi ya dini hiyo, iliyofanyika kwenye makao makuu ya Benki hiyo, jijini Dar es salaam leo.
Mkuu wa Kitengo cha CRDB Al Barakah, Rashid Rashid akizungumza wakati wa hafla yaa uzinduzi wa huduma za bima zinazozingatia misingi ya shariah zijulikanazo kama Takaful kwa ajili ya wateja wanaofuata imani ya Kiislamu na wananchi wengine wanaozingatia misingi ya dini hiyo, iliyofanyika kwenye makao makuu ya Benki hiyo, jijini Dar es salaam leo.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post