MUSWADA UWEKEZAJI UMMA KUFANYIWA MAREKEBISHO

Na Dotto Kwilasa,DODOMA


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) Deus Sangu, amesema kuwa Muswada wa Uwekezaji wa Umma unatarajiwa kupelekwa bungeni ili kufanya marekebisho kwenye ofisi ya msajili wa hazina na kuleta ufanisi kwenye masuala ya uwekezaji binafsi. 

Hayo yamebainishwa bungeni Jijini Dodoma na Mwenyekiti huyo wa PIC wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimisha zoezi la kupokea maoni ya wadau kuhusu sheria hiyo kufutwa na kuongeza kuwa  endapo Muswada huo utapitishwa utasaidia kuanzisha Taasisi ya Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania ambayo itachukua majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Hazina . 

Amesema lengo la muswada huo ni kufanya marekebisho makubwa kwenye ofisi ya msajili wa hazina ambayo ilikuwa na majukumu ya kusimamia mashirika ya umma 304 japo Mashirika hayo hayajaonesha tija kwenye mapinduzi ya uwekezaji. 

Licha ya hayo amesema tangu kuanzishwa kwa ofisi ya msajili wa hazina kumekuwa na ombwe kwenye uendeshaji wa mashirika ya umma hivyo juhudi zaidi inahitajika ili kuleta tija.

"Serikali imewekeza na kuonesha mfano kwenye maeneo mengi lakini suala la uwekezaji hasa binafsi bado halijatiliwa mkazo inavyohitajika,kuanzishwa kwa mfuko wa uwekezaji kutasaidia kuvutia wawekezaji binafsi ,baada ya mchakato huu sasa tunaingia kwenye hatua ya kuchakata tuje mawazo ya kupeleka bungeni, "amesisitiza

Pamoja na hayo amesema iwapo Bunge litaridhia kupitisha muswada huo Ofisi ya Msajili wa Hazina itafutwa na kuanzisha   Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania ambayo itakuwa na dhima  kusimamia kwa ukaribu mashirika ya umma. 

Sangu amesema ," Kwa mujibu wa takwimu zilizopo hadi kufikia Juni mwaka jana kulikuwa na mashirika ya umma  304 ingawa tija inayokusudiwa  bado imekuwa iko chini,Serikali imewekeza zaidi ya sh.trilioni 76.7 katika mashirika hayo ambapo fedha hizo ni bajeti ya miaka miwili ya nchi, "amesema na kuongeza;

“Lengo  la serikali ni  kuona uwekezaji unakuwa na tija katika maeneo mbalimbali pamoja na  kuwa kichocheo kikubwa cha uchumi kwa sababu ndiyo muwekezaji mkubwa,”amesema.

Aidha Mbunge huyo wa Jimbo la Kwela (CCM) amesema baada ya muswada huo kupitishwa utaanzisha Mfuko wa Uwekezaji ambapo itahakikisha mashirika yote yanakuwa na mitaji ya kutosha kwa ajili ya kujiendesha.

Amesema wamepokea maoni ya wadau zaidi ya 50 na tunaendelea kupokea kupitia ofisi ya Bunge baada ya hapo kamati itakaa kwa ajili ya kuyachakata na kuwasilisha ndani ya bunge ili kuridhia kuwa sheria kamili ambayo itaanzisha taasisi mpya, "amesema.

Ameongeza kuwa ”Tunaamini sheria hii ikipita kutakuwa na mambo mazuri ikiwemo wakurugenzi wa bodi za taasisi kutewuliwa kwa njia ya ushindani ambapo na wale wenye sifa ndio watapata nafasi.


 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post