'KALAMU' YA KIBOSHO ILIVYOZALISHA WASOMI HADI MAPROFESA

Na Deogratius Temba - Moshi

KALAMU sio kitu kipya kwa watu wote, unaposikia neno ‘Kalamu’ kinachokujia kichwani ni ile inayotumika kuandikia kwenye karatasi au sehemu nyingine.

Huko Kibosho Moshi,mkoani Kilimanjaro, wanawake wafanyabiashara wadogo wa ndizi mbivu, wanaotokea maeneo ya Kibosho Kirima , kwao kalamu ni aina ya Kibox ambacho hutumika kubeba ndizi mbivu, kilichotengenezwa kwa ustadi mkubwa na fundi seremala kwaajili ya kumwezesha kujitwisha kichwani na kusafiri nachO hadi Moshi mjini kwaajili ya kuuza ndizi. Kalamu hutumika kutunza usalama wa mikungu ya ndizi zisiharibike.

Hivi karibuni, wakati wa mapumziko ya sikukuu za Noeli (Krismas), nikakutana na Mama anayeitwa Maria Modest, ambaye ni mwenyeji wa Kibosho - Kirima masoka ambaye anaitumia ‘kalamu’ kuuzia ndizi zake.
Nilimuuliza, ni kwanini hii inaitwa ‘kalamu’? akasema “kwani hujui? Hii ilitumika tangu zamani sana, Bibi zetu ndio walikibatiza hiki kibox jina hilo” akasema Maria akifikiri kwamba mwandishi ni mgeni sana eneo hilo.

Mwandishi: kwanini hao kina Bibi wa zamani, wajasiriamali walikiita jina hilo? 

Maria akajibu: “Ahaaaa, sasa ni kuambie, hao kina Bibi, walitusimulia kwamba walikiita hivyo kwa sababu walifanya biashara hii ya ndizi kwa kubeba kichwani na wakafanikiwa kuwasomesha watoto wao hadi wakafika vyuo vikuu”

Mwandishi: Ehheee! Hadi Vyuo vikuu kabisa? Ada inapatikana kwa hii biashara?

Maria: Mhhhh, yaani mwanangu nikuambie, hata mimi ni shahidi, nimesomesha watoto wangu shule nzuri, wapo wawili, mmoja ameshamaliza Chuo Kikuu, na sasa amepata kazi, huyo mdogo wake yupo Chuo kikuu kingine, ninalipa ada shilingi 1,600,000 kwa biashara yangu hii, na mimi nina pata mahitaji yangu yote na matibabu” anaeleza maria kwa kujiamini.

Lakini maria anaeleza kwamba, wanawake wengi hapo awali hawakuamini kwamba biashara ile ya kubeba ndizi kichwani itawakomboa, lakini kwa kuona wanawake wa Kibosho –Kirima Boro waliofanikiwa waliamua kuiga na sehemu nyingine.

Anaeleza kwamba, wakiwa wanashangaa wale wanaotokea maeneo ya Boro wanavyofanikiwa, wale wanaotokea maeneo ya Kirima Masoka, walikuja kuiga biashara hiyo na sasa wamefanikiwa sana.

“Mimi ninazaliwa kule Boro, lakini nimeolewa Masoka, kule Boro biashara hii ipo sana, wanawake karibia wote wenye afya nzuri wanafanya biashara hizi, upatikanaji wa ndizi mbichi kwaajili ya kufundika ni wa shida, lakini huku masoka ndizi zipo maana awali hakukuwa na ushindani mkubwa wa wanawake anaozifundika”, anasema Maria.

Jitihada za wanawake wengi kufanya biashara kwa lengo la kujikombia kiuchumi zinafanikiwa kwa jinsi wao wenyewe wanavyoweka mtazamo chanya juu ya kile wanachokifanya wakiamini kwamba kitaleta tija. Suala muhimu ni serikali kuweka mifumo rafiki ya kuwawezesha kufanya biashara na kukutana na wateja wao bila kusukumwa, kunyang’anywa biashara zao na mgambo, au maafisa wengine.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post