DC MKUDE ATOA WIKI MOJA WANAFUNZI WAWE SHULENI, MAGANZO SEKONDARI SITA TU WAMERIPOTI


Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude akifundisha mtoto aliyeripoti katika shule ya msingi Maganzo kwa ajili ya kuanza darasa la awali namna ya kuunda herufi

Na Eunice Kanumba,Kishapu.

Mkuu wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Joseph Mkude ameonesha kutoridhishwa na kasi ya ndogo ya wanafunzi kuripoti katika shule ya sekondari Maganzo iliyopo kata ya Maganzo wilayani humo mkoani Shinyanga ambapo kati ya wanafunzi 594 waliochaguliwa kujiunga na shule hiyo ni wanafunzi 6 ndio wameripoti siku ya Jumatatu Januari 8 huku kati hao wasichana wakiwa na wanne na wavulana wawili.

Akizungumza mara baada ya kufika shuleni hapo Januari 8, 2024 kufuatia ziara yake ya ukaguzi wa shule mbalimbali wilayani humo ili kujionea uandikishwaji wa wanafunzi katika shule za awali na msingi pamoja na mahudhurio kwa wanafunzi wote waliotakiwa kuripoti shuleni ili kuanza masomo ya kidato cha kwanza.

Kufuatia hali hiyo, Mkude amewapa wiki moja viongozi katika eneo hilo kuwatafuta wanafunzi wote ambao hawajaripoti ili wafike shuleni hapo kwa ajili ya kuanza masomo.

“Wanafunzi ambao ndiyo wenye shule hawataki kuja shuleni siku ya kwanza ili shule afungue nani? wafungue walimu ? hilo halikubaliki ninachotaka diwani uitishe kikao cha wenyeviti wote wa vijiji na vitongoji mshughulikie suala hili , hivyo natoa muda wa wiki moja watoto wote waotakiwa kuanza masomo waripoti shuleni”, amesema Mkude.

Aidha Mkude amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa sana kwa kuweka mazingira wezeshi na rafiki katika upatikanaji wa elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa ya kisasa na mazuri hivyo katika katika kuunga mkono maendeleo hayo wananchi hawana budi kuwaruhusu watoto kuripoti shuleni na kuanza masomo mara moja ili kutengeneza kizazi cha uelewa kwani wanafunzi wa leo ndiyo viongozi wa baadaye.

Kwa upande wake Afisa elimu kata ya Maganzo Nkinga Ngoyeji amesema hali ya kuripoti kwa wanafunzi katika shule ya sekondari Maganzo hairidhishi kwani wanafunzi karibu wote waliotakiwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza shuleni hapo hawajaripoti shuleni hapo ukitoa hao sita pekee huku akitoa wito kwa wazazi wa wanafunzi hao kuwaruhusu watoto hao kufika shuleni hapo kwa ajili ya kuanza masomo vinginevyo sheria itachukuliwa dhidi ya wazazi wa watoto hao kwa kufikishwa mahakamani.

“Ni kweli hali ya kuripoti kwa wanafunzi kwa ajili ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza kwa mwaka huu 2024 si nzuri kabisa kwani wameripoti wachache ambao ni sita tu kati ya wanafunzi 594 ,changamoto kubwa watoto ni watoro kinachofuata tunatafuta utaratibu wa kisheria kwa kuwakamata wazazi wote wa watoto ambao hawajaripoti shule ni ili sheria ichukue mkondo wake”, amesema Ngoyeji.

Akizungumzia hali hiyo, Diwani wa kata ya Maganzo Mbalu Kidiga amesema ili kutatua changamoto hiyo katika kata ya Maganzo anakwenda kuitisha kikao cha wenyeviti wa vijiji na vitongoji kwa kushirikiana na jeshi la sungusungu ili kufanya msako na kuwabaini wazazi wote ambao watoto wao hawaripoti shuleni ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa na watoto hao waweze kuripoti shuleni na kuanza masomo.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post