WANAOJISAIDIA VICHAKANI HAWANA VYOO WATAJWA KUSAMBAZA KIPINDUPINDU KISHAPU, RC MNDEME ASEMA WATU SITA WAMEFARIKI


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme (katikati) akiwa katika kata ya Idukilo wilaya ya Kishapu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme.
Mganga Mkuu wa Serikali Prof; Tumaini Nagu.

Na Kadama Malunde - Shinyanga

Nyumba ni choo! Ndivyo inavyojulikana. Hata hivyo imebainika kuwa bado kaya nyingi Wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga hazina vyoo hali imetajwa kuwa chanzo cha kusambaa kwa ugonjwa wa kipindupindu ambao tangu ulipozuka mwezi Desemba 2023 watu sita mkoani humo wamethibitika kufariki dunia huku idadi ya wagonjwa ikiongezeka kutoka 18 hadi kufikia 139.

Akiwa katika kata ya Idukilo wilayani Kishapu wakati wa ziara yake leo Jumanne Januari 23,2024 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme aliyekuwa ameambatana na ameambatana na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu ameeleza kusikitishwa na kata kukosa vyoo hivyo amemwagiza Mkuu wa wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude pamoja na Watendaji wote wa Serikali kufanya msako na kuwapiga faini wananchi ambao hawajajenga vyoo na wataogoma kulipa faini wafikishwe mahakamani.

Akizungumza na wananchi katika kukabiliana na ugonjwa wa Kipindupindu, Mhe. Mndeme amesema kaya 142 katika kata hiyo ambako ndiyo chimbuko la ugonjwa wa Kipindupindu kwa Wilaya ya Kishapu hazina vyoo hali ambayo imekuwa ikisababisha wananchi wake kujisaidia vichakani na kusababisha uchafu kuingia kwenye mto Tungu ambao maji yake yanatumiwa na wananchi kwa shughuli mbalimbali hivyo kuwa chanzo cha kusambaa ugonjwa huo.


“Kaya 142 kukosa vyoo ni aibu kubwa kwa viongozi kuanzia ngazi ya Vitongoji na Vijiji. Hapa nimeuliza mkatoa taarifa ya uongo kuwa kuna vyoo, acheni kudanganya kwenye suala la afya, kamateni weka ndani watu wote wasio na vyoo hakuna muda wa kulea mtu sasa, lazima tukomeshe jambo tatizo hili”, amesema Mhe. Mndeme.

Ameeleza kuwa ugonjwa wa Kipindupindu umeshamiri katika kijiji cha Idukilo kwa kusababishwa na wananchi wenyewe kwa kushindwa kuchimba vyoo na matokeo yake wanajisaidia hovyo jambo ambalo halikubaliki na kubainisha kuwa wanataka kukomesha tatizo hilo.

"Mkuu wa wilaya na watendaji wote wa Serikali kumbe ilitolewa siku wananchi hawa katika Kata hizi 142 wawe wameshajenga vyoo na leo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho, hivyo hakuna kuongeza siku ya kujenga vyoo na msako huu uanze mara moja wasiona vyoo piga faini ambao hawana peleka mahakamani ugonjwa huu siyo muda wa wa kuchekeana",amesema Mndeme.

Mtendaji wa Kata ya Idukilo Maryciana Robert amesema awali walishapitisha sheria ndogo na kutoa maagizo kwamba kwa wananchi wote ambao hawana vyoo hadi kufikia leo Januari 23, 2024 wawe wameshajenga vyoo na ambao bado watapigwa faini ya Sh. 50,000 na ambao hawatatoa watafikishwa mahakamani.


Akielezea kuhusu changamoto ya maji katika Kijiji cha Idukilo, Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Kishapu Mhandisi Dickson Kamazima amesema awali wananchi walikuwa hawana maji kutoka na genereta kuharibika lakini kwa sasa huduma imerejea ambapo sasa wananchi wanapata huduma ya maji kupitia kisima kirefu chenye urefu wa mita 130 na kinauwezo wa kuzalisha lita 12,000 kwa saa na kinahudumia zaidi ya watu 4000 wa Vijiji vitatu Kata ya Idukilo.

Naye Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amesema hakuna upungufu wa vifaa tiba kwani serikali imetoa dawa za kutibu maji katika Mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa inayokabiliwa na tatizo la ugonjwa wa kipindupindu zaidi ya milioni saba lakini pia wametoa vifaa kinga vya watumishi wanaotoa huduma kwa wagonjwa na maji tiba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments