RAIS SAMIA NI MFANO WA KUIGWA BARANI AFRIKAChama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kuwa Mwenyekiti wa CCM, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni mfano wa kuigwa kwa vijana wa Afrika, wakiwemo wa kike wanaotaka kuwa mahiri na kujenga ushawishi mkubwa katika maeneo mbalimbali ya uongozi kadri ya ndoto zao.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Anamringi Macha, Dusemba 12, 2023, alipokuwa akitoa salaam za CCM kuwakaribisha viongozi vijana wanawake kutoka nchi 16 barani Afrika, wanaoshiriki Mkutano wa Mwaka wa Taasisi ya Young Women of Africa (YWOA), unaofanyika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha, mkoani Pwani.

“Tunapozungumza muda huu kutoka hapa tulipo kuna idadi kubwa ya wanawake katika nyanja mbalimbali za maisha ambao wamefanikiwa kubadilisha mtazamo na mwonekano wa jamii kuhusu wanawake, katika nchi zao, Afrika na dunia kwa ujumla, hasa kutoka kwenye mtazamo dhaifu na kuwa mtazamo wa uimara na umakini.”

“Wamekuwa mfano wa kuigwa kwa namna ambavyo wameweza kudhihirisha pasipo shaka yoyote kuhusu uwezo na nguvu za mwanamke.”

“Kwenye nyanja ya siasa, hapa tunaye Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, ambaye umahiri, uimara na uwezo katika uongozi, unatambuliwa na kukubalika duniani kote sasa. Wiki iliyopita tu, Jarida la Forbes limemtaja kuwa ni mmoja wa wanawake 100 wenye nguvu na ushawishi mkubwa duniani,” amesema Ndugu Macha.

Akiwasisitiza kuhusu umuhimu wa kujiamini kwa kutumia dhana ya uwezo wa mwanamke, kuliko kujikita kwenye udhaifu zaidi, Ndugu Macha pia aliwapatia mfano wa Mgombea Urais wa Chama cha SWAPO cha Namibia kwenye uchaguzi mkuu wa nchi hiyo mwaka kesho, akiwaambia kuwa ni mfano mwingine wa jinsi ambavyo wanawake wanapaswa kubadili mitazamo ya dhana dhalili.

“Tunapozungumza hapa, wenzetu SWAPO wa Namibia, wanajiandaa na uchaguzi na mgombea wao wa Urais ni mwanamke…kwa hiyo nao wanajiandaa kutufuata sisi Tanzania kwa kuwa na Rais mwanamama. Mifano hii tunayo kwenye nyanja zote za maisha sasa, hata zile zinazoendesha dunia, iwe kwenye kisiasa, iwe taaluma, michezo na zingine zote utakazoweza kusema. Kwenye chumba hiki tuna mfano wa Profesa Marcellina Chijoriga. Mnaona jinsi anavyosimamia na kuendesha shule hii kwa viwango na muonekano wa kimataifa,” amesema Ndugu Macha.

Alitoa wito kwa viongozi vijana wanawake kutokuwa wanyonge katika kuhakikisha wanatimiza ndoto za mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali katika maisha yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post