MVUA KUBWA YA MAWE NA UPEPO YAANGUSHA NYUMBA 51 SHINYANGA... MASHAMBA YAHARIBIWA


 Na Marco Maduhu. 

Mvua ya Mawe na Upepo imeleta maafa katika Kijiji cha Ibanza Kata ya Mwamala wilayani Shinyanga ambapo nyumba 51 zimeanguka na kusababisha wananchi kukosa makazi, pamoja na kuathiri mashamba na mifugo.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Desemba 6,2023 majira ya saa 9 usiku.

Mmoja wa waathirika wa tukio hilo Jilala Dutu, amesema mvua ilianza kunyesha majira hayo ya usiku huku wakiwa wamelala, lakini ghafla walisikia mabati yakibebwa na upepo na kutupwa pembeni na nyumba yao, na wakati huo huo nyumba ikianguka kwa ndani na kujeruhi mtoto na Mama Mkwe wake.

“Nyumba ilivyoanguka tofali lilimpiga mtoto kichwani akachanika, huku mama mkwe naye akipigwa na tofali na kuvunjika mguu lakini hakuna kifo ambacho kimetokea,”amesema Dutu.

Akieleza maafa yaliyotokana na mvua hizo Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Simon Berege, amesema nyumba 51 zimeanguka, mashamba ya mahindi Hekari 10 yameathirika, kuku 20 wamekufa na mbuzi mmoja amekufa na hakuna kifo, na Bibi ambaye amevunjika Mguu anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme aliyefika eneo la tukio, ametoa pole kwa waathirika wote wa mvua hiyo, huku akibainisha kuwa kwa wananchi ambao wote wameumia Serikali itagharamikia matibabu yao.

Amesema mbali na kugharamia matibabu, pia wananchi ambao mashamba yao yameharibika watapewa mbegu bure ili wapande upya kwa sababu mvua bado zinaendelea kunyesha,na kubainisha kuwa wale ambao watahitaji Maturubai watapewa, na kuwapongeza wananchi ambao wamejitolea kuwahifadhi ndugu zao kwa muda.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post