HUDUMA BORA ZITOLEWE KWA UMMA KWA MAENDELEO ENDELEVU - MAONGEZI

 


Na. Gideon Gregory, Dodoma.

Kaimu Katibu, Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma, Celina Maongezi, ametoa rai kwa waajiri wote, mamlaka za ajira na nidhamu kuhakikisha wanasimamia vyema sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili kuhakikisha huduma bora zinaendelea kutolewa kwa umma kwaajili ya maendeleo endelevu.

Maongezi ametoa rai hiyo leo Desemba 8,2023Jijini Dodoma wakati akiambatana na baadhi ya viongozi wa taasisi simamizi kukagua namna taasisi zilizojitokeza kutoa huduma katika wiki ya maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu yanayoendelea Jijini humo.


“Taasisi za umma zimepewa dhamana na Serikali kuhakikisha kuwa zinatekeleza au zinatoa huduma bora kwa wananchi, kwamaana hiyo niwajibu sasa kwa kila mamlaka ya nidhamu, mamlaka ya ajira na waajiri wote kuhakikisha kwamba wanapotekeleza majukumu yao kuhakikisha wanafuata taratibu, sheria, kanuni na miongozo iliyopo,”amesema.

Kwa upande wake mkurugenzi msaidizi, idara ya usimamizi wa maadili Ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na Utawala Bora Ally Ngowo amesema kuwa katika ukaguzi walio ufanya siku ya leo wamebaini kuwa eneo la ardhi ndiyo limekuwa na watu wengi kutokana na kuwepo changamoto mbalimbali kuhusiana na ardhi.

“Pamoja na njia nyingine ambayo Wizara husika imekwisha kuziandaa nmna ambavyo wateja wanaweza kuwasilisha malalamiko yao na bahati nzuri hapa Dodoma tuna kliniki ya Ardhi inaendelea katika ofisi za wizara mkoa hivyo nitumie wasaha huu kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kutatuliwa changamoto zao,”amesema.

Nao baadhi ya washiriki waliojitokeza katika maonesho hayo wamesema muitikio wa wananchi ni mkubwa huku changamoto kubwa ikiwa ni uelewa mdogo kuhusiana na taasisi hizo namna ambavyo zinafanya kazi.


Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu yalizinduliwa Desemba 3 waziri wa katiba na sheria Balozi Dkt. Pindi Chana huku kilele chake kitakuwa Disemba 10 katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma na yanaongozwa na kauli mbiu ya ‘’Mapambano Dhidi ya Rushwa ‘’Zingatia Maadili, Utu, Uhuru na Haki kwa Watu Wote kwa Maendeleo Endelevu’.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post