NGOMA ZA UNYAGO ZACHANGIA MIMBA ZA UTOTONI KIBAHA


Na Mwandishi wetu

Uwepo wa ngoma za jadi wanazochezwa wasichana wadogo kwa jamii ya Mkoa wa Pwani kumechangia uwepo wa ndoa na mimba za utotoni na kusababisha wasichana kuhsindwa kufikia ndoo zao ikiwepo kuwa viongozi katika jamii.

Akizungumza wakati wa zoezi la mrejesho wa uraghibishi (PAR), kwa viongozi wa Kata ya Pangani, Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mkoani Pwani, Diwani wa kata hiyo, Augustino Mdachi, alisema kwamba Mimba za utotoni zinasababishwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa mila na desturi zinazopelekea watoto wa kike kuingizwa kwenye mazingira ya vishawishi na hatarishi.

Aidha, Diwani huyo amesema pia, sababu nyingine ni umbali wa kupata elimu ya sekondari kwani wanafunzi wanatembea umbali mrefu kutoka mitaa ya Vikawe Bondeni na Vikawe shule kwenda shule ya sekondari Kidimu iliyoko makao makuu ya Kata.

Uraghibish huo ambao unahusisha utafiti shirikishi wa jamii, umefanywa na shirika lisilo la kiserikali la Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), kama sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa kuwezesha sauti za wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu, katika uongozi na haki ya kumiliki rasilimali, unaofadhiliwa na shirika laUmoja wa Mataifa linaloshughuikia masuala ya wanawake (UNWomen) katika halmashauri hiyo.

TGNP na UNwomen wanashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, kujenga uwezo kwa jamii, kujitambua, kubadilisha mitazamo, mila na desturi ambazo zinachangia wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu, kushindwa kushiriki kwenye nafasi za uongozi na maamuzi katika ngazi mbalimbali na kuangalia vikwazo vinavyochangia kundi hilo kutokumiliki rasilimali.

“Tatizo la Umbali ni chanzo cha hizi mimba za utoto ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa wasichana kupoteza ndoto yao ya kupata elimu na kuja kuwa viongozi wa kesho. Mfano wasichana wanaotembea umbali wote kutoka Vikawe hadi Kidimu ni tatizo kubwa na linaweza kusababisba mimba. Tunaendelea na utaratibu,tumeshaanza mchakato wa kupata shule nyingine ya sekondari Vikawe ili kuondoa tatizo hilo”

Aidha, washiriki wa Utafiti huo walipendekeza kwamba, endapo wazazi watawalinda watoto wa kike, kwa kuzuia ushiriki wao kwenye ngoma za unyago, na kuhakikisha wanaochezwa unyago ni wale waliofikia umri wa ujana na utu uzima, tatizo la mimba za utotoni litakoma. Pia walipendekaza kuzuia wasichana wanaochezwa ngoma za unyago kutokutolewa ndani wakiwa kifua wazi kwani inawadhalilisha na kuwakosesha ujasiri wa kuwa viongozi au kusimama mbele za watu.

Naye mwenyekiti wa Mtaa wa Vikawe Anas Bwanari, alisema kwamba kwenye mtaa wake mimba za utotoni ni tatizo kubwa ambapo sababia anazo ziona yeye ni kutokana ana migogoro ya ndoa, uwepo wa talaka, ambapo watoto wanalellewa na mzazi mmoja au kulelewa na wazazi wa kufikia ambao pia huwafanyia vitendo vya Ukatili wa KIjinsia.

“vitendo vya Ukatili wa Kijinsia vinasababisha wanawake kushindwa kufikia malengo yao, ikiwepo kumiliki rasilimali, kunufaika na rasilimali zilizopo na kuwa viongozi wazuri wa kesho. Tunashauri uwepo wa elimu yakujitambua kwa jamii nzima, ili kuondoa tatizo la mimba za utotoni, lakini pia kupunguza Ukatili wa Kijinsia kwa wanawake”alisema

Awali akitoa maelezo juu ya zoezi hilo lilofanyika, Mwezshaji wa uraghibish kutoka TGNP, Deogratius Temba, alisema kwamba, baada ya kuwaongoza wanajamii kufanya uraghibish masuala mbalimbali yameibuliwa na kupangwa katika vipaumbele, ambapo suala la Uongozi usiowajibika, Mimba za utotoni na mila na desturi kandamizi yalionekana ni sababu ya wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu kushindwa kushiriki kikamilifu kwenye nafasi za uongozi na maamuzi na pia katika umiliki wa rasilimali.

Uraghibishi unaofanywa na TGNP, unalenga kuijenga jamii, katika mtzamo wa kiuchambuzi kwa kuibua fursa na changamoto zinazowazunguka, kuchambua sababu za wazi, za kina kiini cha tatizo, na kuweka mikakai ya kutekeleza au kutoa mapendekezo ya utatuzi wa tatizo.

Ni dhana inayotumika kuibadilisha jamii kutoka katika mtazamo wa kuitegemea serikali kufanya kila kitu, na kuifanya jamii kupendekeza njia zao za utatuzi kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka kwa kushirikiana na viongozi. Na pia inaondoa migogoro kati ya jamii na viongozi wao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post