BARRICK NORTH MARA YAPONGEZWA KUUNGANA NA WADAU MBALIMBALI KUFANIKISHA MAADHIMISHO YA KILELE CHA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA 2023Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt .Yahaya Nawanda, akihutubia wakati wa maadhimisho ya kilele cha Kampeni ya Kitaifa ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia yaliyofanyika Nyamongo wilayani Tarime, Desemba 10, 2023.
Mkurugenzi wa Jinsia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Badru Abdunuru, akizungumza wakati wa maadhimisho hayo
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko, akizungumza wakati wa maadhimisho ya kilele cha Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia.
Msafara wa Kampeni ya Kitaifa ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia wakifuatilia jambo wakati wa maadhimisho ya kilele cha kampeni hiyo.
Viongozi wa Serikali, Kampuni ya Barrick na Shirika la WiLDAF Tanzania katika picha ya pamoja mara baada ya kukabidhi kitabu cha mwongozo wa kupinga na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, wakati wa maadhimisho ya kilele cha Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia.
****

Maadhimisho ya kilele cha Kampeni ya Kitaifa ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia kwa Mwaka 2023, yamefanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Nyamongo wilayani Tarime, chini ya udhamini wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara.

Kupitia maadhimisho hayo, Serikali imelikabidhi Shirika la WiLDAF Tanzania kitabu cha mwongozo cha Kampuni ya Barrick Gold kuanzisha klabu za vijana za maendeleo marafiki wa North Mara.

Aidha, Kampuni ya Barrick imetumia fursa hiyo kuzindua vilabu vya Marafiki wa North Mara, katika shule 10 za sekondari zilizopo maeneo yanayozunguka mgodi huo.

Mgeni rasmi katika maadhimisho alikuwa ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt. Yahaya Nawanda, ambaye katika hotuba yake alipongeza mgodi wa Barrick North Mara na wadau wengine waliofanikisha kampeni hiyo.

Dkt. Nawanda ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote wanaopambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, kwa ustawi wa maendeleo ya jamii nzima.

Amelihimiza Jeshi la Polisi kuhakikisha watu wote wanaojihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia, ukiwemo ukeketaji wanakamatwa na kuchukulia hatua kali za kisheria. “Ukeketaji hauna nafasi katika karne hii,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jinsia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Badru Abdunuru, amesema Serikali inaendelea kuongeza uwekezaji kwenye mipango ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, miongoni mwa changamoto nyingine.

Abdunuru, ambaye alimwakilisha, Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Dorothy Gwajima, naye ameipongeza Barrick na mashirika mengine yaliyosaidia kufanikisha kampeni hiyo ya siku 16 za za kupinga ukatili wa kijinsia, akisema itasaidia kuongeza msukumo wa kuchukua hatua za kutokomeza vitendo hivyo katika jamii.

Alisema Serikali inaendelea kuongeza uwekezaji kwenye mipango ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, miongoni na changamoto nyingine.

Mwakilishi wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, Jean Clark, amesema maadhimisho ya kilele cha kampeni hiyo yana umuhimu mkubwa kwani yamefanyika siku ambayo pia ni ya Maadhimisho ya Miaka 75 ya Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu (GM) wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko, amesema Mgodi huo unatambua juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kupinga ukatili wa kijinsia, ndio maana haukurudi nyuma kusaidia kufanikisha maadhimisho hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, yeye ameomba waratibu wa kampeni ya kitaifa ya kupiga vita ukatili wa kijinsia kuangalia uwezekano wa kupiga kambi wilayani humo mwakani kwa ajili ya kukemea vitendo vya ukeketaji vinavyotarajiwa kufanyika miongoni mwa jamii ya kabla la Wakurya.

Awali, Anna Kulaya, ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la WiLDAF Tanzania, lililoratibu Kampeni ya Kitaifa Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia, amesema kampeni hiyo ilizinduliwa na Waziri Gwajima, Novemba 25, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Kulaya ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali na mashirika yote yaliyojitokeza kuliunga mkono shirika lake kwa hali na mali katika kufanikisha kampeni hiyo.


“Tunatoa shukrani za dhati kwa Barrick - wametushika mkono sana katika kampeni hii, wamekuwa wadau wakubwa, na mgodi wao wa North Mara umewekeza sana katika kuzuia ukatili wa kijinsia. Vilabu vya Marafiki wa North Mara vilivyoanzishwa vitachochea kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia katika jamii inayouzunguka,” amesema.

Mkurugenzi huyo wa WiLDAF Tanzania ameweka wazi kuwa waliamua maadhimisho ya kilele cha kampeni hiyo yafanyike mkoani Mara kutokana na mkoa huo kuongoza kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Kiongozi wa msafara wa watu 18 wa kampeni hiyo, Idd Mziray, amesema wamefanikiwa kupita katika mikoa mbalimbali ikiwemo Morogoro, Dodoma, Kigoma, Kagera, Geita na hatimaye Mara.

Mziray ametaja taasisi walizopita kwa ajili ya kutoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kuwa ni pamoja na shule za msingi na sekondari, misikiti na makanisa.


Maadhimisho hayo ya Kilele cha Kampeni ya Kitaifa ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia kwa Mwaka 2023, yenye kaulimbiu inayosema: “Wekeza Kuzuia Ukatili wa Kijinsia”, yamehudhuriwa pia na askari polisi, viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, makundi tofauti ya wananchi, wakiwemo wanafunzi na wazee wa mila.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post