WATUMIAJI MAJI YA MVUA WATAHADHARISHWA

Meneja Uhusiano na Masoko,Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA)Athuman Sharif 

Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Meneja Uhusiano na Masoko,Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA)Athuman Sharif amewashauri wananchi wanaopendelea kutumia maji ya mvua kuwa na uelewa mpana wa uvunaji, uhifadhi na matumizi sahihi ya maji hayo  kuepuka maradhi yatokanayo na vumbi, moshi na gesi mbalimbali zikiwamo carbon dioxide, oxygen na nitrogen dioxide ambazo si salama kiafya.

Hayo yameelezwa leo November 13,2023 Jijini Dodoma na meneja huyo wakati akizungumza na Waandishi wa habari ikiwa ni sehemu ya uelimishaji wa umma kuhusu namna bora ya uvunaji na matumizi sahihi ya maji ya mvua. 

Amesema licha ya faida lukuki za maji ya mvua,bado maji hayo si salama ikiwa hayakidhi viwango vya ubora unaotakiwa wa kuongeza madini na kwamba kabla ya kuyatumia lazima maji hayo yachanganywe na maji ya vyanzo vingine ili kuwa na madini yanayohitajika na kuepusha magonjwa yasiyo lazima. 

"Kuna watu hawafaham matumizi sahihi ya maji ya mvua,maji haya yana sifa nyingi na yamepoa
utumia maji ya mvua kwa usahihi unahitajika kwa kuzingatia kuvuna katika vyombo safi, kuhifadhiwa kwa usafi kwenye tanki  ambalo haliruhusu mwanga au hewa kwa sababu Maji ya mvua yanapopata mwanga huzalisha gesi na kuzalisha wadudu wanaoharibu ubora wa maji, "amesema

Amefafanua kuwa, " Kwa asili maji ya mvua kabla hayajafika katika anga letu huwa ni safi na salama kwa kunywa,hata hivyo, maji hayo lazima yapite katika anga na ndipo yafike ardhini kama mvua,hapo ndipo hatari ya maji ya mvua inapoanza na kuongezeka zaidi yanapofika katika paa la nyumba au sehemu maalumu iliyojengwa kuvuna maji hayo na hatimaye kuhifadhiwa katika ndoo au tenki, "amesema

Mbali na hayo ameshauri maji hayo yachemshwe kabla ya kuyatumia kwa kunywa au kupiga mswaki na kusisitiza kuwa wanaovuna maji ya mvua wanapaswa kupima maji yao katika maabara za maji pale wanapoyavuna na miezi kadhaa baada ya kuyahifadhi ili kuua bakteria. 

"Maji  hayo yanapoingia katika chombo cha kuhifadhia yanaweza kuwa mazalia mazuri ya vijidudu vinavyosababisha magonjwa ya tumbo kama vile kuhara, homa ya tumbo, kipindupindu na hata kuzalisha mbu wanaoeneza magonjwa mbalimbali mfano malaria, 

"Kiwango kidogo cha madini katika maji ya mvua kinayafanya maji hayo kukosa ladha ukilinganisha na maji ya kisima, mto, ziwa au bomba,watu wanashauriwa waanze kukinga au kuvuna maji dakika tano baada ya mvua kuanza kunyesha ili paa la nyumba au sehemu ingine inayotumika kukusanya maji ijisafishe kwa mvua ya kwanza, "amesisitiza na kuongeza;

"Kiasi kidogo cha madini kama calcium, magnesium, iron, na fluoride ni muhimu katika maji ili kuimarisha afya. Katika baadhi ya nchi, maji ya mvua husafishwa na kuongezwa madini muhimu kiafya na kusambazwa kwa wananchi kama maji ya kunywa, " amesema

Kwa wanaongeza chumvi kwenye maji mvua Meneja huyo ameshauri kuwa, "Kuweka chumvi si vizuri kwa kuwa kuna baadhi ya chumvi hazina madini ya Iodine,kiasili maji yote ni masafi, lakini yanaweza kuchafuliwa ,tumia maji haya mpaka uwe unafahamu viwango vya madini yake au kutokana na ushauri wa mamlaka za maji RUWASA, ''amesisitiza

Kutokana na hayo baadhi ya watumiaji wa maji ya mvua mkoani hapa wameeleza faida ya uvunaji wa maji hayo kuwa ni pamoja na kukidhi uhaba wa maji,kilimo na uhifadhi wa mazingira hasa maeneo yaliyo hatarini kukabiliwa na athari mbaya  ukame na jangwa. 

James Nzige ameeleza kuwa uhifadhi wa maji ya mvua ni muhimu kwa kuwa huleta faida kwenye kilimo cha umwagiliaji na utunzaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na kusaidia malisho ya wanyama wanaofugwa. 

"Ukiyaacha maji yatiririke bila utaratibu husababisha mmomonyoko wa tabaka la juu la ardhi yenye rutuba ya udongo na  kuleta mafuriko,kiasi cha maji kuwa chini  na kupungua kwenye udongo wenye rutuba hufanya iwe ngumu kukuza mazao, na kusababisha uhaba wa chakula hii inaweza kusababisha njaa hivyo uhifadhi maji ya mvua ni uhai wa kilimo na mazingira, "amesema

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post