WAKANDARASI WABABAISHAJI WASIPEWE KAZI BASHUNGWA.
Na Oscar Assenga,TANGA


Waziri wa ujenzi Innocent Bashungwa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kuhakikisha kuwa wakandarasi wasumbufu na wababaishaji hawapewi kazi za ujenzi wa barabara nchini kote.


Akizungumza alipokagua Barabara ya Handeni-Mafuleta 20km Bashungwa amesema ni aibu kuwa na mkandarasi msumbufu anaechelewesha kazi na bado kupewa miradi mingine hali inachelewesha maendeleo kwa wananchi.


Alimuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini kuhakikisha Mkandarasi huyu HHEG hapewi mradi nyengine ya km 30 mpaka watakapojiridhisha na kasi yake ya ujenzi wa km 20 alizonazo sasa ifikapo Januari mwakani

Alisema haiwezekani mkandarasi anapewa kazi ya mradi wa km 30 na hakamilishi kwa wakati na bado wanafikiria kumpa eneo nyengine suala hilo haliwezi kukubalika hata kidogo


Aidha Waziri Bashungwa alimtaka Mtendaji Mkuu wa Tanroad kuhakikisha wanajipanga vizuri na kusimamia wataalam wake ili Barabara ziweze kukamilika kwa wakati

" Wana ujenzi wote tuwahudumie watanzania kwa kutanguliza uzalendo mbele," amesisitiza Waziri Bashungwa"

Waziri huyo amezungumzia umuhimu wa wakandarasi kuwa na uhusiano mzuri na wananchi katika ni maeneo wanayofanyia kazi kwani kufanya hivyo ni sehemu ya ulinzi kwenye miradi wanayoitekeleza.


Katika hatua nyengine Waziri Bashungwa amemuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga Eng. Eliazari Rweikiza kuhakikisha HHEG anayejenga Barabara ya Handeni-Mafuleta anaboresha barabara inayotumika kati ya Handeni na Kilindi ili kupunguza kero ya usafiri kwa wananchi.

"Lakini Mtendaji Mkuu wa TANROADS hakikisheni katika vipaumbele vya barabara zitakazojengwa kwa lami iwe ni pamoja na barabara za Handeni-Mziha -Turiani( KM 108.2), Kiberashi-Songe (KM 33.5)na Songe-Gairo ili kuufungua vizuri mkoa wa Tanga hususan wilaya za Handeni na Kilindi"Alisema


Awali akizungumza katika ziara hiyo Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Mohammed Besta alimueleza Waziri huyo kwamba tayari TANROADS wameshawapanga mameneja wa miradi katika miradi yote 69 inayoendelea nchini ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ubora unaotakiwa.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Handeni mjini Mh.Ruben Kwagirwa amempongeza Waziri wa ujenzi kwa miradi mbalimbali ya barabara inayoendelea mkoani Tanga na kusisitiza kwamba kufunguka kwa barabara ya Mkata -Kwamsisi (Km 36), Handeni Turiani (KM 108.2), Handeni- Kiberashi- Singida, (KM434), Kiberashi- Songe ( KM 33.5) na Songe -Gairo kutaufungua vizuri mkoa wa Tanga na kuuunganisha na makao makuu ya nchi Dodoma kwa njia fupi.

Waziri Bashungwa yupo katika ziara ya kukagua athari za mvua za vuli mkoani Tanga na kukagua miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja inayoendelea mkoani Tanga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post