TUMUENZI MWALIMU NYERERE KWA VITENDO

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Mwegoha (kulia), akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Dennis Mwila (kushoto), ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya katika Kongamano la Miaka 20 ya Kumbukizi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. 

*******************

Wito umetolewa kwa jamii ya watanzania kuenzi fikra na falsafa za Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuwa zinaishi na kuendelea kuwa funzo kwa vizazi na vizazi.

Haya yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Kanali Dennis Mwila wakati wa Kongamano la miaka 20 ya Kumbukizi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyoandaliwa na Chuo Kikuu Mzumbe na kufanyika Jijini Mbeya.

Amesema ni dhahiri kuwa falsaza za mwalimu katika kuenzi rasilimali za Taifa na Utawala bora ni wazi kwani misingi iliyowekwa tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza inasimamiwa mpaka sasa.

"Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni kiongozi aliyeweka msingi wa uhuru wetu na kuimarisha nchi yetu na leo tunatambulika ulimwenguni kote kutokana na mchango wake mkubwa wa kuikomboa Tanzania na Afrika kwa ujumla wake" amesisitiza Homera.

Kwa upande wake Mzee Joseph Butiku Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere ambae pia alikuwa ni mtoa Mada Mkuu katika Kongamano hilo amesema Mwalimu Nyerere ameacha mafundisho mengi katika utawala bora na usimamizi wa rasilimali za nchi.

"Sote ni mashahidi Mwalimu Nyerere katika maisha yake amekuwa akisisitiza misingi ya uongozi wa kiadilifu, uwajibikaji na ushirikiano wa wananchi katika kufikia malengo ya maendeleo. Leo, tunahimizwa kuchukua mafundisho haya kama mwongozo katika shughuli zetu za kila siku" Amesisitiza Mzee Butiku.

Akiongea na jumuiya ya wafunzi walioshiriki katika Kongamano hilo ametoa rai kwao kutumia elimu na maarifa wanayopata katika kujenga kesho yao ili kuwa na Taifa lenye vijana wenye misingi ya uzalendo, uwajibika na kujitegemea.

Awali, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha amesema Chuo hicho kinajivunia kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuzalisha wataalamu wenye maadili na maarifa katika eneo la utawala na utawala bora.

"Tunaendelea kufundisha na kutoa elimu inayojikita katika misingi ya uwajibikaji, uwazi na usimamizi thabiti wa rasilimali za umma. Tunawaanda vijana wetu kuchota hekima za Mwalimu Nyerere na kuwajengea uwezo wa kuwa viongozi wa baadae wanaozingatia maadili na maendeleo endelevu" Prof. Mwegoha amefafanua.

Katika kongamano hilo jumla ya mada ndogo sita ziliwasilishwa na wanazuoni kutoka Chuo Kikuu Mzumbe na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwa ni Mtazamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu masuala ya Ardhi, Wanawake, Madini, viwanda na kuongozwa na kaulimbiu isemayo "Mtazamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu utawala bora na ulinzi wa rasilimali za taifa kwa maendeleo endelevu"

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Dennis Mwila (Kulia), Mgeni Rasmi wa Kongamano la Miaka 20 ya Kumbukizi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akisalimiana na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere na Mzungumzaji Mkuu wa Kongamano, Mzee Joseph Butiku (kushoto).

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Dennis Mwila, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya katika ufunguzi wa Kongamano la Miaka 20 ya Kumbukizi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lililofanyika jijini Mbeya na kuratibiwa na Chuo Kikuu Mzumbe.

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Dennis Mwila (katikati), Mwakilishi Wa Mgeni Rasimi wa Kongamano la Miaka 20 ya Kumbukizi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Mwendeshaji Mkuu wa Kongamano Dkt. Ayoub Rioba na Mtoa mada Mkuu wa kongamano hilo Mzee Joseph Butiku

Mkurugenzi Mkuu wa TBC, na Mwongozaji Mkuu Wa Kongamano la 20 la Kumbukizi ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Dkt. Ayoub Rioba, akizungumza wakati wa kongamano hilo.

Mhadhiri kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Richard Mbunda, akitoa mada juu Mtazamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu Ulinganifu wa Usimamizi wa rasilimali na mabadiliko ya serikali za Tanzania.

Mhadhiri wa Sheria Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya, Dkt. Tasco Romanus Luambano, akitoa mada juu Mtazamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu rasilimali madini na utawala bora.

Mhadhiri Mwandamizi wa Taasisi ya Taaluma za Maendeleo, Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Lulu Elizabeth Genda, akitoa mada juu Mtazamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu Jukumu la wanawake katika kulinda rasilimali za Taifa.

Mhadhiri Mwandamizi wa Taasisi ya Taaluma za Maendeleo, Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Theobald Frank Theodory, akitoa mada juu Mtazamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu makadirio na mwelekeo wa maendeleo ya viwanda nchini tanzania.

Wanafunzi na washiriki mbalimbali wakiuliza maswali na kuchangia mada wakati wa kongamano la 20 la Kumbukizi ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lililofanyika Mbeya hivi karibuni na kuratibiwa na Chuo Kikuu Mzumbe.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe - Mipango, Fedha Na Utawala, Prof. Allen Mushi, akitoa neno la shukrani wakati wa kuhitimisha Kongamano la 20 la Kumbukizi Ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lililofanyika Jijini Mbeya hivi karibuni

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post