MAKATIBU WAKUU WAFANYA ZIARA HANDENI WANAPOHAMIA WAKAZI WA NGORONGORO


Makatibu Wakuu wakikagua maendeleo ya ujenzi nyumba na miundo mbinu ya kuhamisha wananchi wanaotoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni  wakati wa ziara yao mkoani Tanga.

Na Mwandishi wetu - Tanga

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi Dkt. Yonazi amesema Serikali imejipanga katika kuhakikisha kuwa wizara zote za kisekta zinashiriki kikamilifu katika kuhakikisha kuwa miradi iliyopo katika Kijiji cha Msomera inakamilika kwa wakati ili kuwezesha wananchi wanaoendelea kujiandikisha kuhamia katika eneo hilo ili kuendelea shughuli zao. 

Dkt. Yonazi aliyasema hayo wakati  wa ziara ya kikazi  ya Makatibu Wakuu wa Wizara za kisekta waliyoifanya katika  Kijiji cha Msomera, Wilaya, Handeni mkoani Tanga kujionea hatua mbalimbali za ujenzi wa miundombinu  kabla ya kuanza kwa awamu ya pili ya kuhamisha wananchi wanaoishi katika hifadhi ya Ngorongoro waliojiandikisha kuhama kwa hiari.

Amesema Makatibu Wakuu  hao wamekagua ujenzi wa miundo mbinu mbalimbali ikiwemo maji, umeme, madaraja, barabara, shule, Nyumba za makazi na uboreshaji wa huduma za mawasiliano.

“Niwaombe wanaohamia eneo hili waiamini Serikali kwamba inawatengenezea mazingira yaliyo bora sana hapa Msomera, nyumba  zinazojengwa  na huduma zote zina ubora ili wananchi wetu wanufaike  na Serikali yao waachane na upotoshaji kwa sababu imewekeza fedha nyingi kuhakikisha wanaishi katika mazingira salama,”Amesema Dkt. Yonazi.

Naye  Kamanda wa Kikosi  Kazi cha Ujenzi wa nyumba 5000  kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema kila taasisi ya kisekta na Wizara  zinawajibika ipasavyo kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati  akisema kuwa  licha ya changamoto za mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali lakini kazi inaendelea vizuri .

“Mpaka sasa ujenzi wa Msomera  ambao tumeugawanya katika vitalu kuanzia A mpaka D tuko katika hatua mbalimbali za ujenzi nyumba 1000 katika eneo la Msomera B kitalu F viwanja 768  taratibu zake zimekamilika eneo liko tayari kwa ajili ya uchimbaji na kuanza msingi na kuendelea na hatua za ujenzi,”Ameeleza Brigedia Jenerali Mabena.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Albert Msando  amewashukuru Makatibu Wakuu hao kwa kutembelea mradi huo hatua inayoongeza kasi yake kusonga mbele akiahidi kusimamia kwa karibu mradi huo ambao umefanyika kama hatua ya kuboresha maisha ya watanzania kila mwananchi kuishi katika hali ya ustawi pamoja na uwepo wa miundo mbinu muhimu pamoja na huduma za kijamii.

“Hii inaonyesha nia ya dhati ya Serikali  ya kukamilisha mradi huu muhimu kwa wakati siyo tu kuhamisha watu lakini unaenda kuboresha maisha ya watanzania tunaendelea kuwaahidi kwamba tutasimamia kwa karibu tunajua unatekelezwa wakati wa mvua ambapo kwetu ni fursa ya kuona namna ya kuyavuna maji  kwa ajili ya matumizi,”Amebainisha  


Aidha Mwenyekiti wa Kijiji cha Msomera Bw. Martin Oleikayo Paraketi amempongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya mradi huo akisema umekuja kwa wakati muafaka kwani umesaidia  wakazi waliokuwa wakiishi katika maeneo hayo kupata huduma muhimu zikiwemo mawasiliano, ujenzi wa shule za sekondari, kituo cha afya na barabara.

“Hii kwetu ni neema kubwa sana Serikali inafanya kazi kubwa na niwaambie waliopo Ngorongoro wasikubali kupotoshwa na watu wachache wasio na nia njema  kijiji cha Msomera ni kijiji mojawapo  kati ya Vijiji 91 ndani ya Wilaya ya Handeni mradi huu umeleta faida kubwa kupitia wenzetu waliohamia kutoka Ngorongoro,”Amepongeza Mwenyekiti huyo.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post