e-GA YATAKA WACHAMBUZI MIFUMO YA TEHAMA KUWA WABUNIFUNa Dotto Kwilasa,Dodoma

Wachambuzi wa mifumo ya TEHAMA ‘Business Analysts’ katika taasisi za umma, wametakiwa kuongeza elimu na kupata maarifa mapya mara kwa mara, ili kuweza kuendana na kasi ya ukuaji wa mabadiliko ya teknolojia mpya zinazoibuka, ikiwemo ujuzi katika uchambuzi wa takwimu pamoja na akili bandia.

Wito huo umetolewa na Kaimu Meneja wa Ushauri na Uelekezi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bi.Joan Valentine, wakati akifungua mafunzo ya siku sita kwa Wachambuzi wa mifumo ya TEHAMA yanayofanyika katika ofisi za Kambarage Tower jijini Dodoma.

Aidha, Bi. Joan aliwataka Maafisa hao kujifunza stadi mbalimbali ikiwemo teknolojia ya akili bandia na uchambuzi wa takwimu, ili ziwasaidie kupambana na mabadiliko ya teknolojia yanayoibuka duniani mara kwa mara na kuhakikisha teknolojia hizo zinasaidia ukuaji wa taasisi zao.

“Kwa sasa dunia inazungumza kuhusu akili bandia, hivyo wachambuzi wa mifumo lazima muwe na ujuzi wa hizi teknolojia ili kuzisaidia taasisi zenu katika utendaji kazi wa kila siku”, alisema Bi.Joan.

Vilevile, aliwataka maafisa hao kuona umuhimu wa kujifunza stadi tepe ‘soft skills’ ili ziweze kuwasaidia katika kupambana na mabadiliko yanayoendelea kutokea katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ulimwengu kote.

“Kwa sasa TEHAMA inatoka kuwa fani saidizi ‘supporting tool’ hadi kuwa fani wezeshi ‘enabling tool’ hivyo, mnatakiwa muwe wajuzi zaidi katika sekta ya TEHAMA ili kuzisaidia taasisi zenu katika kupiga hatua katika utendaji kazi wa kila siku”, alisisitiza.

Mratibu wa Mafunzo hayo Bw.Ceaser Mwambani ambaye pia ni Mchambuzi wa Mifumo ya TEHAMA e-GA, alisema kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Maafisa hao, katika maeneo ya Uchambuzi wa Mifumo ya TEHAMA, Usimamizi wa Miradi ya TEHAMA, Miongozo, Viwango, Usimamizi, Ubora na Usalama wa Mifumo ya TEHAMA Serikalini.

“Kupitia mafunzo haya, tunaimani kuwa, washiriki wote hapa watakuwa na uelewa zaidi kuhusu uchambuzi wa mifumo na miradi ya TEHAMA Pamoja na kuweza kutoa mchango mzuri kwenye taasisi zao ili kuwa na miradi yenye tija kwa taifa”, alifafanua.

Mafunzo hayo yanayotarajiwa kukamilika Novemba 25, mwaka huu ikiwa ni muendelezo wa jitihada za e-GA za kuhakikisha inashirikiana na kuzijengea uwezo taasisi za umma katika kukuza Serikali Mtandao.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post