WATALAAMU WA UHIFADHI WA MALIASILI NA UTALII WAPIGWA MSASA KUFANYA TAFITI ZA KISAYANSI


Na. John Bera

Wizara ya Maliasili na Utalii imeendesha mafunzo kwa watumishi wa Wizara, taasisi mbalimbali za serikali na vyuo vikuu kuhusu namna bora ya kufanya tafiti zitakazosaidia kuondoa changamoto na kuimarisha uwekezaji katika maeneo ya uhifadhi nchini.

Akizungumza leo Jijini Dodoma wakati wa mafunzo ya namna ya kufanya tafiti kuhusu uhusiano wa watu na uhifadhi yaliyoendeshwa na wataalamu wabobezi kutoka Chuo Kikuu cha Bangor cha nchini Uingereza, Mkurugenzi wa Mafunzo na Utafiti  kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Edward Kohi amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka na kwamba mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara, vyuo na taasisi zake njia sahihi za kufanya tafiti zinazohusisha watu haswa kama ni suala lenye utata.

Aidha, Dkt. Kohi amesema mafunzo hayo yatakuwa endelevu katika kuhakikisha kazi nzuri inafanyika katika kutambua changamoto za uhifadhi kwa kutumia nyenzo sahihi katika kukabiliana na changamoto hizo. Alifafanua Zaidi kwa kusema  katika mafunzo hayo washiriki wanajifunza uandaaji mzuri wa dodoso kwa kuandaa na kuuliza maswali na namna ya kuchakata maswali na takwimu zinazopatikana wakati wa kufanya tafiti. 

"Mafunzo haya yanaleta nyongeza ya eneo la saikolojia kwenye tafiti zinazohusisha watu na uhifadhi, na njia mbali mbali za kuandaa maswali ambayo watu wengi huwa na mashaka kuyajibu kiurahisi kama vile ‘umetumia kiasi gani ukiwa hifadhini, umeshawahi winda hifadhini? n.k." 

"Mafunzo haya yamekuja wakati sahihi ambapo mkakati wa kutekeleza Sera ya Wanyamapori ya mwaka 2007 inafanyiwa maboresho hivyo mafunzo yatachangia watafiti kupata matokeo na taarifa sahihi za utafiti zitakazoongoza na kusaidia kuboresha sera mbalimbali za uhifadhi, kutatua changamoto na pia yatasaidia katika kufanya uwekezaji  na taarifa zinazotuongoza katika kutoa maamuzi makubwa katika sekta ya uhifadhi na utalii."

Kwa upande wake, Mshiriki kutoka Idara ya Misitu na Nyuki, Dkt. Siima Salome Bakengesa amesema kupitia mafunzo hayo wanajifunza namna ya kutumia taarifa sahihi kutoka kwa watu wanaoishi maeneo yanayopakana na hifadhi.

"Tunaamani baada ya mafunzo haya tutakuwa na uwezo wa kufanya tafiti ambazo zitaendelea kutusaidia katika uhifadhi maeneo yetu ambayo tunahifadhi kwa misitu na wanyama." 

Naye Dkt. Agnes Carol Kisanga kutoka Idara ya Baiolojia Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) amesema kupitia mafunzo hayo wanajifunza njia tofauti tofauti ya kufanya tafiti wa kujua namna ya kuendelea kuhifadhi.

“Hii ina maana kwa sasa tunakwenda kuhamia kufanya tafiti kwa kutumia sayansi ya saikolojia na sayansi ya jamii kwa kupeana maoni ya watu tofauti na inayofanyika sasa.”

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na  Washiriki 25 kutoka Wizara ya Maliasili  na utalii  (TAFORI, TAWIRI, Idara ya wanyamapori, Idara ya Sera na Mipango, Kitengo cha Utafiti na Mafunzo na Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) ikiwemo washiriki kutoka  Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na taasisi ya COLBAT Ltd.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post