WADAU WA UCHAGUZI WATAKIWA KUWAHAMASISHA WANACHI KATA YA IKOMA WILAYANI RORYA KUSHIRIKI UBORESHAJI



Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Ramadhani Kailima akifungua mkutano wa Tume na wadau wa uchagaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mapsap Linme iliyopo wilayani Rorya Mkoa wa Mara.
Wakili wa Serikali Mkuu Kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bi. Rose Chilongozi akisoma mada ya uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye mkutano wa wadau wa uchaguzi wilayani Rorya.

Baadhi ya washiriki wa mkutano wa Tume na wadau wa uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mapsap Linme iliyopo wilayani Rorya Mkoa wa Mara.

Baadhi ya washiriki wa mkutano wa Tume na wadau wa uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mapsap Linme iliyopo wilayani Rorya Mkoa wa Mara.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Ramadhani Kailima (wa pili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa vyama vya siasa baada ya kumalizika kwa mkutano wa Tume na wadau wa uchaguzi.

************
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewataka wadau wa uchaguzi kufikisha ujumbe sahihi kwa wananchi wa Kata ya Ikoma katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ili wananchi wenye sifa ya kuandikishwa na kuboresha taarifa zao wajitokeze kwa wingi kushiriki uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuwabainisha waliopoteza sifa za kuwa wapiga kura.


Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Ramadhani Kailima wakati akifungua mkutano wa Tume na wadau wa uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mapsap Linme iliyopo wilayani Rorya Mkoa wa Mara.


Aliwaasa wadau wote wa uchaguzi kuendelea kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika kipindi chote cha uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.


“Ni tegemeo la Tume kuona mnafikisha ujumbe sahihi kwa wananchi ambako uboreshaji wa majaribio yatafanyika ili wananchi wenye sifa ya kuandikishwa na kuboresha taarifa zao wajitokeze kwa wingi kushiriki zoezi hili na kuwabainisha waliopoteza sifa za kuwa wapiga kura.


Pia, nawaasa wadau wote kuendelea kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika kipindi chote cha uboreshaji wa majaribio la Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.”, alisema Bw. Kailima.


Mbali na kuwaasa wadau hao wa uchaguzi, Mkurugenzi wa Uchaguzi alisema kuwa Tume imejipanga kuhakikisha kuwa wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu uboreshaji wa majaribio kwa kutumia njia mbalimbali za kutoa elimu ya mpiga kura zikiwemo; kukutana na wadau wengine wa uchaguzi.


Aliongeza kuwa vyama vya siasa vitashiriki katika uboreshaji wa majaribio kwa kuweka wakala mmoja katika kila kituo cha kuandikisha wapiga kura, lengo ni kushuhudia na kujiridhisha juu ya taratibu zitakazotumika wakati wa uboreshaji wa majaribio wa Daftari.


Alisisitiza kwa kuwaomba wadau wa uchaguzi kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni na mapendekezo kwenye mkutano huo ili kufanikisha utekelezaji wa uboreshaji huo.


Mkutano huo wa wadau wa uchaguzi umewashirikisha viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, wazee wa kimila, watu wenye ulemavu, wawakilishi wa vijana, wawakilishi wa wanawake na asasi za kiraia kwa ujumla kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.


Tume ya Taifa ya Uchaguzi itafanya uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kata ya Ikoma iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoa huu wa Mara na Kata ya Ng’ambo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, mkoa wa Tabora, utakaofanyika kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post