CHUO CHA TAIFA CHA UTALII (NCT) KUTOA MAFUNZO KWA WATOA HUDUMA TRENI YA SGR


Na: Mwandishi wetu, DAR


Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC) wamezindua mafunzo maalum kwa watumishi wa Shirika hilo watakaotoa huduma mbalimbali katika treni ya SGR inayotarajiwa kuanza safari zake hivi karibuni kutoka Jijini Dar es Salaam hadi Morogoro.


Mafunzo hayo ya wiki mbili yanalenga kuwajengea uwezo maafisa hao katika utoaji wa huduma bora na zenye viwango vya Kimataifa katika treni hiyo.

Akizungumza katika hotuba yake wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Novemba 11, 2023 Jijini Dar es Salaam, Makamu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), Taaluma, Utafiti na Ushauri Jesca William, amesema mafunzo hayo yanafanyika katika Kampasi ya Bustani ya Chuo hicho Jijini Dar es Salaam, na kwamba Chuo hicho kinatambua umuhimu wa Sekta ya usafirishaji katika masuala mazima ya Utalii.

"Sekta ya usafirishaji imeendelea kuwa nguzo muhimu katika uchumi wa Tanzania, hivyo tunapaswa kuendelea kuboresha huduma tunazozitoa kwani mtalii ni msafiri pia.

"Kupitia uboreshaji wa huduma za usafirishaji kwa njia ya Reli, kutachangia pia kuboresha huduma kwa watii na kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi" amesema Jesca.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu Rasilimali watu na Utawala Amina Lumuli amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka fedha nyingi katika kutekeleza Miradi ya Kimkakati ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ambao unaenda kuleta mapinduzi makubwa katika Sekta ya usafirishaji na kuimarisha uchumi wa nchi.

"Mradi huu wa SGR Kipande cha kwanza cha Dar es Salaam hadi Morogoro umekamilika kwa asilimia 98.60 na hivi karibuni tumepokea kichwa cha kwanza kinachotumia umeme kwaajili ya kuanza rasmi majaribio.

"Hivyo, Shirika la Reli ambalo linatekeleza Mradi huu halina budi kujiandaa ipasavyo ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa na viwango vya Kimataifa" amesema Amina.

Aidha amesema kuwa mafunzo hayo ya huduma kwa wateja awamu ya kwanza yanahusisha jumla ya watumishi 70 ambao ni wauza tiketi, Mapokezi, wahudumu wa ndani ya treni, Stesheni Masta pamoja na watumishi wa huduma kwa wateja.

Amewataka washiriki wote wa mafunzo hayo kuwa na weledi wa kutosha ili kupata ujuzi utakao wezesha kutoa huduma bora na zenye hadhi ya Kimataifa kwani Mradi huo utavutia watu wengi wakiwemo watalii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post