MKAKATI WA ACHIA SHOKA KAMATA MZINGA WAIVA, WADAU WA NYUKI WATAKIWA KUJIPANGA NA APIMONDIA 2027


Na John Mapepele

Kamati ya kitaifa ya Kuandaa Mpango Kabambe  wa kuendeleza Sekta ya Ufugaji wa Nyuki nchini unaojulikana kama “Achia Shoka Kamata Mzinga” leo Novemba 16,2023  imewasilisha rasimu  ya mpango huo kwa wadau wa sekta hiyo baada ya kukamilisha kazi ya kuuandaa na  kupata maoni nchi nzima ili uende mbela kwa  hatua zaidi.

Mpango huo  wa  Achia Shoka, Kamata Mzinga umelenga kuweka mazingira wezeshi ya wananchi kunufaika na rasilimali za nyuki na misitu na kuboresha uzalishaji na uuzaji wa asali ndani na nje ya nchi ambapo kwa sasa Tanzania inazalisha tani 32000 wakati uwezo wake ni tani138000 kwa  mwaka.


Akifungua warsha hii ambayo imewajumuisha wadau wote kwenye mnyororo wa thamani wa uzalishaji wa asali nchini ya kupokea maoni ya rasimu ya Mpango huo, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi, Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo, Dkt. Edward Kohi amesema warsha  hiyo imewashirikisha wabobezi wote wa sekta na amewasihi watumie nafasi hiyo kuchangia mawazo yao ili kupata mpango utakaokuwa mwarobaini wa changamoto zinazokabili sekta hiyo kwa sasa.


"Pamoja na uwepo wa mikakati na jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau wa sekta binafsi, bado kiwango cha uzalishaji wa asali na mazao mengine ya nyuki na biashara ya asali hasa katika masoko ya nje ya nchi hakiridhishi hivyo tutumie warsha ya leo  kutengeneza kitu ambacho  kitakuwa na faida kwa kizazi cha sasa na baadaye  kama ambavyo kauli mbiu ya wizara inavyosema kuwa tumerithishwa tuwarithishe”, amefafanua Dkt. Kohi.


Amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuona kuwa mpango huu unaleta  mapinduzi makubwa katika sekta ya ufugaji nyuki na kuongeza mchango wa sekta ya nyuki katika Pato la Taifa


Aidha, amesisitiza kuwa  wakati umefika kwa wadau  kuangalia  namna ambavyo mdudu nyuki anavyoweza kuhifadhiwa  vema na kutumika katika utalii wa nyuki ambao  ukiendelezwa vizuri utaliingizia taifa.

Pia Dkt. Kohi amewataka wadau wote wa nyuki nchini kujipanga na kuona  namna ambavyo wanaweza kunufaika na mkutano mkubwa wa kidunia  wa wadau wa nyuki (Apimondia) utakaofanyika nchini 2027.

Makundi yaliyoshiriki warsha hiyo ni kutoka kwenye taasisi na maeneo ambayo shughuli za ufugaji nyuki zimeshamiri, ikijumuisha wafugaji nyuki, wachakataji na wafanyabiashara wa mazao ya nyuki, maafisa ufugaji nyuki wilaya, wadhibiti ubora, watafiti, wanazuoni, wataalamu, wasimamizi na watunga sera.


Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki ambaye pia ni Katibu wa Kamati hiyo na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Misitu na Nyuki Daniel Pancras aliishukuru Wizara na wadau  kwa kuendelea kuweka misingi  thabiti ya usimamizi wa raslimali za Misitu na Nyuki na kuandaa mpango huo.


Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Mkabwa Manoko amemhakikishia mgeni rasmi kuwaanaamini uwezo mkubwa wa wadau utasaidia  kutoa maoni yao kwa weledi ili kukiwezesha kamati yake  kukamilisha kazi kwa wakati.


Katika kilele cha Siku ya Nyuki Duniani Mei 21,2023 mkoani Singida,  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania Mhe,Dkt. Philipo I. Mpango aliielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kuandaa  mpango huo, ndipo wizara ikaunda Kamati Maalum kwa ajili ya kazi hii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post