WAZIRI NDALICHAKO AWATAKA WAAJIRI KUWEKA MIFUMO ENDELEVU YA KUFANYA MAZOEZI KWA WAFANYAKAZI WAO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof.Joyce Ndalichako akizindua kilele cha Waajiri Bonanza 2023 leo Oktoba 7,2023 katika Viwanja vya Leaders Jijini Dar es Salaam.

*****************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof.Joyce Ndalichako amewataka waajiri nchini kuweka mifumo endelevu ambayo pamoja na kufanya kazi pia itawapa fursa ya kuimarisha afya zao ikiwemo kuweka programu za mazoezi.

Waziri Ndalichako ametoa wito huo leo Oktoba 7,2023 Jijini Dar es Salaam wakati akifunga bonanza la Afya la Waajiri kwa mwaka 2023 lililofanyika katika Viwanja vya Leaders, bonanza lililobeba ujumbe unaosema “Kuimarisha Afya ya Akili ili Kuongeza Tija Mahali pa kazi”.

Aidha Waziri Ndalichako ameipongeza Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kufanya bonanza la Afya la Waajiri kwa mwaka 2023 kwani linakwenda kuimarisha afya na kuwaweka karibu waajiri kutoka katika maeneo mbalimbali.

Waziri Ndalichako amewataka waajiri kuhakikisha wanachukua hatua kuhakikisha wafanyakazi wanapata nafasi ya kushiriki michezo kwani ni njia nzuri ya kuboresha afya ya akili.

"Uzalishaji wenye tija unatokana afya njema ya wafanyakazi hivyo ni bora kahakikisha wafanyakazi wanakua na afya njema. Waajiri wekeni mkazo katika kuhakikisha wafanyakazi wanakua na afya njema ya akili ili kuongeza ufanisi kazini". Ameeleza

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi. Suzanne Ndomba amesema kuwa jumla ya makampuni 150 yameshiriki Bonanza hilo ambapo kati yao 50 wameshiriki michezo, 15 wameweka mabanda na kuonyesha biashara zao.

"Tangu kuanza kwa bonanza na maonyesho ya huduma kwa wateja tarehe 5 mpaka leo ambapo ni kilele takribani watu 2000 na zaidi wameshiriki". Amesema

Amesema kuwa ATE ilianza kuratibu Bonanza la Waajiri mwaka jana ikiwa na lengo la kuwakutanisha Waajiri na wafanyakazi kwa Pamoja kufanya mazoezi na kujadili masuala ya afya na usalama mahala pa kazi.

Nae Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa Ofisi ya Afrika Mashariki, Bi. Noreen Toroka amesema kuwa ILO itaendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali akiwemo ATE, TUCTA, OSHA, WCF, NSSF, PSSSF na Serikali kuunga mkono programu za kukuza Ajira sambamba na kuzingatia Usalama na Afya mahali pa Kazi.

Bonanza la leo lilianza asubuhi kwa Mazoezi ya Viungo(Aerobics) kwa washiriki wote na kufuatiwa na michezo mingine kama vile mpira wa miguu (Football), Mpira wa Pete (Netball), Mpira wa Kikapu, Kuvuta kamba, Kukimbia na ndimu kwenye kijiko, Kukimbia na Magunia, pamoja na kukimbia na glasi ya maji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof.Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa kufunga bonanza la Afya la Waajiri kwa mwaka 2023 lililofanyika leo Oktoba 7,2023 katika Viwanja vya Leaders Jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi. Suzanne Ndomba akizungumza wakati wa kufunga bonanza la Afya la Waajiri kwa mwaka 2023 lililofanyika leo Oktoba 7,2023 katika Viwanja vya Leaders Jijini Dar es Salaam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post