***************
-Lengo ni kusaka watalaamu watakaotumika katika masoko ya mitaji, sekta ya fedha
Na Mwandishi Wetu, Michuzi Blog
WANAFUNZI zaidi ya 18000 kutoka taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu wameshiriki Shindano la Masoko ya Mitaji na kati yao washiriki 20 wamepata alama za juu, watakutana na jopo la timu ya watalaamu ili kuulizwa maswali na watakaoibuka washindi watapata zawadi mbalimbali.
Hitimisho la shindano hilo linatarajiwa kufanyika Oktoba 26 mwaka huu na mgeni rasmi katika siku hiyo anatarajiwa kuwa Waziri wa Fedha DK.Mwigulu Nchemba ambaye ndiye atakayekabidhi zawadi kwa washindi wa shindano hilo lenye lengo la kutafuta watalaam katika masoko ya mitaji na sekta ya fedha kwa ujumla.
Akizungumza leo Oktoba 23, 2023 jijini Dar es Salaam kuhusu hitimisho la mashindano ya taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA.Nicodemus Mkama amesema ili uweze kuwapata watendaji wanaokidhi viwango vya kimataifa,kwanza unapaswa kujenga elimu na uelewa katika vyuo vikuu hapa nchini , hivyo leo ni siku muhimu katika maendeleo na ustawi wa sekta ya fedha kwani wanao vijana ambao ni washiriki kutoka vyuo vikuu hapa nchini Tanzania Bara na Visiwani.
"Tuliendesha shindano ambalo limeweza kuvutia washiriki zaidi ya 18000 na kati ya hao tumepata washindi waliopata alama za juu, ambapo wao wapo katika wale washindi 20 ikiwa inajumuisha washiriki 102 ambao ni asilimia 0.5 ya washindi wote walioshiriki,
"Kwa hiyo washiriki hawa wanapaswa kukutana na jopo la majaji ambapo jopo hili la majaji lina watalaamu kutoka taasisi mbalimbali fedha zikiwemo benki, watalaam kutoka Taasisi ya Uwekezaji wa Pamoja( UTT) pamoja na Watumishi House.Lengo ni kuhakikisha tunawapata washindi ambao watakidhi vigezo ambavyo watakwenda sasa kupata zawadi zao siku ya Alhamisi",amesema CPA Mkama
Amesema katika hafla hiyo wanatarajia kuwa na mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa Fedha Dk.Mwigulu Nchemba ambaye atatoa zawadi kwa washindi huku akisisitiza shindano hilo ni muhimu,kwani limewezesha kupata watalaam ambao wamekuwa wakitumika kutoa huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa.
Ameongeza kwamba washindi ambao watapatikana watapata zawadi mbalimbali ikiwa pamoja na fedha taslimu lakini vilevile katika fedha watakazopata kiasi cha theluthi moja watawekeza katika hisa za Kampuni ambazo zimeorodheshwa katika Soko la Hisa Dar es Salaam.
Pia washindi wengine watakaopata alama za juu watapata fursa ya kujengewa uwezo katika taasisi mbalimbali za kifedha na kuwajengea mazingira wezeshi yatakayowawezesha baadae kupata ajira katika taasisi hiyo.
"Kwa hiyo hii ni siku muhimu sana katika maendeleo na ustawi wa masoko ya mitaji pamoja na sekta ya fedha kwa ujumla hapa nchini, " amesema CPA Mkama na kuongeza wamekuwa wakisisitiza wanafunzi ile ya nadharia wanayoipata katika vyuo vikuu waitumie katika uhalisia katika masoko ya mitaji.
"Na tumeweza kuona wanafunzi wengi wakiweza kutumia elimu yao ya nadharia ambapo sasa tunawajenga uwezo ili waweze kufanya kazi katika uhalisia katika soko.
"Kwa hiyo tunatoa rai kwa washiriki wote walioshiriki shindano hili kuhakikisha wanajibu maswali yao kwa weledi ili kudhihirisha kwa jopo la majaji kwamba ni kweli wao ndio wameshiriki na kupata alama za juu na hatimaye Oktoba 26 wapate zawadi zao kwa mujibu wa viwango ambavyo watakuwa wamefikia."
Pamoja na hayo amefafanua shindano hilo liko wazi kwa wanafunzi wote walioko katika taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu na katika matokeo ambayo wameyapata kuna wanafunzi ambao hawatoki katika masomo ya biashara au sekta ya fedha lakini wameshiriki.
Baadhi ya hao wanatoka vyuo vya uhandisi pamoja na udaktari ambao wameweza kushiriki na kupata alama za juu, kwa hiyo shindano hilo liko kwa wanafunzi wote Bara na Visiwani na iwapo wataweza kuonesha uwezo wa nadharia katika uhalisia basi watastahili kupata zawadi zitakazotolewa Alhamisi.