SERIKALI KUJENGA MELI MPYA YA MIZIGO KUIONGEZEA UWEZO BANDARI YA KAREMA


Serikali inakusudia kujenga Meli mpya ya Mizigo, Barabara ya Lami na Reli ili kuwezesha Bandari ya Karema iliyopo Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi, iliyokamilika Ujenzi wake kwa Asilimia 100, kufanya kazi kwa uwezo wake wote.

Ahadi hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa alipotembelea Bandari hiyo Jumapili Oktoba 08 2023.

“Nimefurahi kuona Bandari hii nzuri sana, yenye miundombinu ya kisasa na nafasi ya kutoa huduma bora za kibandari kwa Wananchi na Wafanyabiashara wa Nchi za Tanzania, Zambia na Congo DRC”. Amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Mhe.Waziri amesema, ili uwekezaji wa Serikali wa shilingi Bilioni 47.9 uweze kuleta tija, ni lazima ipatikane Meli kubwa ya Mizigo sambamba na ujenzi wa Barabara ya Lami na Reli km. 110 kutoka Mpanda hadi Karema.

Kwa Upande wake Mbunge wa Mpanda Vijijini ambae pia na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Moshi Selemani Kakoso amesema, Wananchi wa Mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma wanamshukuru Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi mkubwa wa Bandari ya kimkakati ya Karema ambayo itainua Uchumi wa Mikoa hiyo kwa kiasi kikubwa ikiwa ni pamoja na kutoa fursa za Ajira kwa Wananchi.

Kwa upande wake Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika Bw. Edward Mabula amesema, tangu kuanza kutumika kwa Bandari ya Karema tarehe 01.09.2022, Abiria 4900 na Tani 1500 za mizigo zimehudumiwa.

Tarehe 11 Oktoba 2023, Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi itasaini Mikataba ya Ujenzi wa Meli mbili za Mizigo zitakazotoa huduma katika Maziwa Victoria na Tanganyika sanjari na Mktaba wa ujenzi wa Karakana ya Meli. Hafla ya utiaji saini huo inafanyika Mkoani Kigoma.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post